Wanawake 50 kuwezeshwa uchumi wa urembo

DAR ES SALAAM: Wanawake vijana 50 wanatarajia kujengewa uwezo na kukuzwa kiuchumi kupitia sekta ya urembo inayokua kwa kasi nchini Tanzania.
Hatua hiyo iMetangazwa leo na Shirika la Her Initiative kupitia mpango wao wa Panda Academy 2026.
Kupitia programu hiyo, wahitimu wamepata mafunzo ya vitendo pamoja na ujuzi wa ujasiriamali na uongozi unaohitajika kuanzisha na kukuza biashara katika utengenezaji wa kucha, bidhaa za ngozi, vipodozi na manukato.
Kwa kipindi cha miezi miwili, washiriki wamepata mafunzo kuhusu ujenzi wa chapa, ufungashaji, uzoefu wa mteja, masoko ya kidijitali, usimamizi wa fedha, uwekaji bei, urasimishaji wa biashara, uzingatiaji wa sheria na maandalizi ya kuingia sokoni.
Mbali na mafunzo hayo, kila mhitimu amekabidhiwa mtaji wa kuanzia biashara kwa njia ya vifaa vya kazi, hatua inayowapa wanawake hao fursa ya kuanza kutekeleza ujuzi walioupata na kujenga biashara zao.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Her Initiative, Lydia Charles Moyo, amesema programu hiyo imelenga kuziba pengo la masoko, mitaji, ujenzi wa chapa na ushauri wa kitaalamu ambalo limekuwa likiwakabili vijana wanawake wenye vipaji vya kutengeneza bidhaa au kutoa huduma.
Amesema dhamira ya programu hiyo inaenda mbali zaidi ya urembo kwa kujenga biashara zinazomilikiwa na wanawake, zinazozalisha kipato, kutengeneza ajira na kuimarisha viwanda vya ndani.
Mmoja wa wahitimu, Tatu Seif Selemani, amesema Panda Academy imemsaidia kubadilisha mtazamo wake na kumwezesha kufikiri kama mjasiriamali, huku akijifunza kutengeneza bidhaa bora, kuzitangaza, kusimamia fedha na kukuza biashara.
Baada ya mahafali, wanawake hao wataendelea kupata msaada kwa miezi miwili ili kuwasaidia kutatua changamoto za biashara na kujiandaa kwa ukuaji.
Kupitia hatua hiyo, Panda Academy inaendelea kutoa fursa kwa vijana wanawake kupata ujuzi, mtaji na mwongozo wa biashara unaoweza kuwasaidia kujenga kipato na kutoa fursa kwa wanawake wengine katika jamii.



