Wawekezaji wapewa fursa riba ya kudumu

DAR ES SALAAM: WAWEKEZAJI katika sekta mbalimbali nchini wanatarajiwa kunufaika na mpango wa hati fungani inayotoa riba ya kudumu ya asilimia 13 kwa mwaka kupitia hati fungani ya Hatua bond.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hati fungani ya Hatua Bond, Mkuu wa Idara ya Hazina wa I&M Bank Tanzania, Patrick Kapela, amesema Hatua Bond ni sehemu ya mkakati wa  kuimarisha soko la mitaji nchini na kuwapatia wawekezaji fursa salama na yenye ushindani ya uwekezaji wa muda mrefu.

Amesema kupitia hatua bond ambayo ni hatifungani ya miaka mitano malipo yatafanyika kila robo mwaka, huku mtaji ukirejeshwa mwishoni mwa kipindi cha miaka mitano.

“Hatua Bond ni hatua nyingine muhimu katika dhamira yetu ya kuendeleza soko la mitaji la Tanzania huku tukiwapatia wawekezaji fursa nzuri na yenye ushindani ya uwekezaji. Kupitia utoaji huu tunakusanya mtaji wa muda mrefu utakaotuwezesha kufadhili biashara, kusaidia ujasiriamali na kuchangia katika mageuzi ya uchumi wa nchi,” amesema.

Amesema fedha zitakazopatikana kupitia hati fungani hiyo zitatumika kuongeza nguvu ya mtaji wa benki, kupanua utoaji wa mikopo kwa biashara na watu binafsi pamoja na kuimarisha ujumuishi wa kifedha.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania, Zahid Mustafa, amesema uzinduzi wa Hatua Bond unaonyesha ukuaji wa benki hiyo na imani yake katika mustakabali wa uchumi wa Tanzania.

Amesema hatua hiyo inadhihirisha dhamira ya benki ya kujenga thamani ya muda mrefu kwa wateja, wawekezaji na uchumi wa taifa kwa kuendelea kutoa suluhisho za kifedha zinazokidhi mahitaji ya soko.

“Hatua Bond imezinduliwa wakati I&M Bank Tanzania ikiwa imefikia hadhi ya Benki ya Daraja la Kwanza (Tier One Bank) na kuvuka thamani ya mali ya zaidi ya Sh trilioni moja.

Ameongeza “Hati fungani hiyo iko wazi kwa wawekezaji binafsi na taasisi, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa Sh 500,000, hatua inayotarajiwa kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji wa hati fungani zenye mapato ya kudumu na kusaidia maendeleo ya sekta binafsi nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button