Watu 250+ kushiriki mbio za VG Fun Run kesho Dar

DAR ES SALAAM: ZAIDI ya washiriki 250 wanatarajiwa kujitokeza katika mbio za Victoria Group (VG) Fun Run 2026, zitakazofanyika kwa mara ya kwanza kesho, Agosti 8, huku maandalizi ya tukio hilo yakifikia asilimia 100.
Mbio hizo zinazofanyika jijini Dar es Salaam zitahusisha kilomita tano na 10, huku washiriki ambao hawatashiriki mbio wakipewa fursa ya kufanya mazoezi ya kupasha mwili joto, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi na kuzingatia afya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya VG Fun Run, Isdori Msaki, alisema; “Tumekamilisha maandalizi kwa asilimia 100. Tunatarajia washiriki zaidi ya 250.”
Alisema mbio hizo zitaanza 12.00 asubuhi katika eneo la VG Park, Ununio kata ya Kunduchi, wilayani Kinondoni.na zitakwenda hadi zahanati ya Mbweni JKT.
Msaki aliwashukuru wadhamini na washirika mbalimbali waliojitokeza kuunga mkono VG Fun Run, akisema mchango wao umewezesha maandalizi ya tukio hilo kukamilika kwa wakati.
Alisema ushiriki wa taasisi hizo unaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi katika kuhamasisha afya, mazoezi na shughuli zinazolenga kuimarisha mshikamano katika jamii.
Kwa upande wa huduma za afya, alisema Heameda Hospital itakuwa eneo la tukio ikiwa na madaktari na wauguzi watakaotoa huduma kwa washiriki na kuhakikisha wanapata msaada wa kitabibu pale utakapohitajika.
Msaki alisema VG Fun Run haikulenga tu kushindana katika mbio, bali pia kujenga utamaduni wa mazoezi, kuhamasisha afya bora, kuimarisha urafiki na kuongeza mshikamano miongoni mwa jamii.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mtendaji Mkuu wa CRDB Foundation, Tuli Mwambapa, ambaye atakuwa sehemu ya uzinduzi wa mbio hizo.
Alisema Victoria Group imeendelea kukua katika kipindi cha zaidi ya miaka 26, ikiwa na wanachama 113 ambao kwa pamoja wanawakilisha familia zenye zaidi ya watu 700 wanaoshiriki shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo jijini Dar es Salaam.
Aidha, alisema viongozi wa Serikali, wafanyabiashara, wataalamu kutoka sekta binafsi pamoja na marafiki wa Victoria Group wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo.
Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika tukio hilo, akisema ni fursa ya kufanya mazoezi huku wakijenga mahusiano na mshikamano katika jamii.



