JKT Tanzania wakuna kichwa kujiimarisha

DAR ES SALAAM. KOCHA Msaidizi wa JKT Tanzania, George Mketo, amesema timu hiyo inatumia mapumziko ya kalenda ya FIFA kwa kufanya maandalizi ya nguvu kwa michezo iliyo mbele ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na DailyNews Digital kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo Dar es Salaam leo Septemba 21, 2026, amesema kuwa benchi la ufundi limeweka mkazo katika kuboresha safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji ili kuongeza ushindani wa kikosi hicho kinacholenga kumaliza ligi katika nafasi nne za juu
Amesema matokeo ya michezo sita iliyopita hayajawa mazuri kwa matarajio yao, baada ya kushinda miwili, kupoteza mitatu na kutoka sare moja.
“Kwa ujumla huo si mwanzo mzuri kwa timu ambayo inalenga kumaliza katika nafasi nne za juu, tunatumia kipindi hiki kurekebisha mapungufu yetu turudi tukiwa imara,” amesema.
Amesema kwa sasa hawana mpango wa kuweka kambi nje ya Dar es Salaam, badala yake wataendelea na maandalizi yao kuelekea mchezo wa Oktoba 9, dhidi ya Fountain Gate jijini Arusha.
Mketo amesema wachezaji wanaendelea na mazoezi na kurejea majumbani, huku timu ikitarajia kurejea kambini kati ya Septemba 25 na 26 na kwamba pia wamemepanga kucheza mchezo wa kirafiki kati ya timu ya Ligi Kuu au Ligi Daraja la Kwanza.



