Serikali yaombwa kuimarisha Chuo cha Ardhi Morogoro

MOROGORO: MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava, ameitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuongeza nguvu katika kuboresha na kupanua Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) ili kiweze kuongeza uwezo wa kuzalisha wataalamu wengi katika sekta ya ardhi.

Aidha, ameitaka Wizara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka utaratibu wa kutumia wataalamu wanaozalishwa na vyuo vya ardhi kusaidia wananchi na jamii kutatua changamoto za ardhi, hatua itakayosaidia kupunguza migogoro inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Mnzava ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO), mkoani Morogoro.

Ameipongeza ARIMO kwa kazi inayofanya ya kuwaandaa vijana kitaaluma licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Nikipongeze Chuo cha Ardhi Morogoro. Pamoja na changamoto zake, kinafanya kazi nzuri ya kuwaandaa vijana ili watumikie Taifa lao,” amesema Mnzava.

Amesema chuo hicho ni taasisi muhimu katika uzalishaji wa wataalamu wa sekta ya ardhi, hivyo ni muhimu kuendelea kuboresha mipango yake ya maendeleo, ikiwemo kutekeleza mpango kabambe wa chuo.

Mnzava amesema kiu ya Kamati hiyo ni kuona mipango madhubuti ikiwekwa na kutekelezwa katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ARIMO.

Amesema anatamani kuona mabadiliko makubwa katika vyuo vya ardhi vya Morogoro na Tabora, ikiwemo kuboreshwa kwa miundombinu, mazingira ya kujifunzia na uwezo wa vyuo hivyo kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kutembelea Chuo cha Ardhi Morogoro na kujionea shughuli zinazofanyika katika chuo hicho.

Dk. Akwilapo ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara itakiangalia kwa karibu Chuo cha Ardhi Morogoro ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu iliyokusudiwa.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button