Akili unde kutumika kupima saratani ya matiti

DAR ES SALAAM: TEKNOLOJIA ya Akili Bandia (AI) imeanza kutumika katika uchunguzi wa saratani ya matiti nchini, baada ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kupata mashine ya kisasa ya mammography yenye uwezo wa kusaidia kubaini mabadiliko ya awali ya ugonjwa huo.
Mashine hiyo mpya, yenye thamani ya Sh milioni 600, inatumia teknolojia ya kisasa ya X-ray ya matiti na imeunganishwa na mfumo wa akili bandia unaosaidia wataalamu kubaini maeneo yanayoweza kuwa na dalili za saratani na kuhitaji uchunguzi wa kina.
Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Diwani Msemo, amesema teknolojia hiyo itaongeza uwezo wa taasisi katika kugundua saratani ya matiti mapema na kuwawezesha wagonjwa kuanza matibabu kwa wakati.
Amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutambua maeneo yenye mashaka wakati wa uchunguzi na kumwelekeza mtaalamu sehemu inayohitaji kuangaliwa kwa umakini zaidi.
“Ni mashine ya kisasa yenye akili bandia ambayo wakati inafanya screening ina uwezo wa ku-identify baadhi ya maeneo yenye matatizo na kumwonyesha msomaji wa picha hapa kuna shida, hivyo aangalie kwa makini eneo husika,” amesema.
Dk Msemo amesema mashine hiyo pia ina uwezo wa kusaidia kuchukua sampuli ya tishu, maarufu kama biopasy, pale inapobainika kuna eneo linalohitaji uchunguzi zaidi.
Amefafanua kuwa biopasy ni mchakato wa kuchukua sampuli ya tishu mwilini na kuipeleka maabara ili kuchunguzwa na kubaini iwapo ina seli za saratani.
Kwa mujibu wa Dk. Msemo amesema takribani asilimia 10 hadi 12 ya wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo wanakuwa na saratani ya matiti huku ikishika nafasi ya pili baada ya saratani ya mlango wa kizazi.

Amesema matumizi ya mashine hiyo yataunganishwa na huduma nyingine za kisasa zilizopo ORCI, ikiwamo PET Scan, inayosaidia kubaini iwapo saratani imesambaa katika sehemu nyingine za mwili.
Dk Msemo amesema ORCI pia imepanga kuwapeleka wataalamu watatu nchini Uturuki kwa ajili ya kupata mafunzo zaidi ya matumizi ya mashine hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uwezo wa wataalamu nchini.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa Radiolojia na mtaalamu wa uchunguzi wa matiti Dk Anganile Kalinga amesema mashine hiyo inaweza kubaini mabadiliko madogo ambayo wakati mwingine hayaonekani kwa kutumia ultrasound kama vile mabadiliko madogo ya muundo wa titi ambayo yanaweza kuwa dalili za awali za saratani.
“Mashine hii inaweza kuona dalili za mwanzo kabisa ambazo tunaweza kuziita microcalcification na mabadiliko madogo ambayo hata ukifanya ultrasound unaweza usiyaone,” amesema.
Ametoa rai kwa wanawake wenye umri wa miaka 40 na kuendelea kutofanya uchunguzi kwa kusubiri kuonekana kwa uvimbe, bali kufika hospitalini kwa uchunguzi wa matiti mara kwa mara.
Dk Kalinga amesema wanaume pia wanaweza kupata saratani ya matiti, ingawa kiwango chake ni kidogo ikilinganishwa na wanawake, akisema wanapaswa kufika hospitalini iwapo watagundua mabadiliko yoyote katika matiti.



