Bandari Dar yahudumia tani milioni 33.7 za mizigo

DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuongeza uwezo wa kupokea na kuhudumia mizigo kutokana na maboresho ya miundombinu na uwekezaji unaolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari.

Akizungumza wakati wa ziara ya viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu katika miradi mbalimbali ya TPA, Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa TPA, Mhandisi Erick Madinda, amesema ongezeko la mizigo limeifanya mamlaka hiyo kuendelea kuboresha magati na miundombinu mingine ya bandari.

Mhandisi Madinda amesema kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inahudumia kiasi kikubwa cha mizigo, ambacho kimefikia takribani tani milioni 33.7.

Amesema mafanikio hayo yanaendana na jitihada za kuongeza uwezo wa bandari na kuhakikisha meli zinahudumiwa kwa muda mfupi, hatua inayosaidia kuongeza ufanisi wa biashara na kupunguza gharama zinazotokana na meli kukaa muda mrefu bandarini.

Amesema miongoni mwa miradi inayotekelezwa ni ujenzi wa matanki 15 ya kupokea na kusambaza mafuta, ambayo yanatarajiwa kupunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini kutoka hadi siku 21 hadi takribani siku saba.

Kwa mujibu wa Madinda, hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za demurrage, ambazo zinaweza kufikia takribani dola 25,000 kwa siku kwa meli, hivyo kuleta nafuu kwa waagizaji wa mafuta na hatimaye kuchangia upatikanaji wa mafuta kwa gharama nafuu zaidi.

Aidha, amesema TPA inaendelea na mipango ya kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga na kuboresha magati, kuongeza uwezo wa kupokea meli kubwa pamoja na kuboresha usafirishaji wa mizigo kwa kutumia reli ya SGR na barabara.

Amesema hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha bandari inakuwa na ufanisi zaidi, inaongeza mapato na kuhudumia Tanzania pamoja na nchi nyingine zinazotegemea bandari hiyo, huku ikiendelea kuwa kitovu muhimu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa upande wao, viongozi wa wanafunzi waliotembelea bandari hiyo, Oswad Maganya, Rais wa Chuo Kikuu cha Ardhi, na Caren Mary, Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamesema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza kuhusu historia ya maendeleo ya Bandari ya Dar es Salaam na mwelekeo wake wa baadaye.

Wamesema maarifa waliyoyapata yatawasaidia katika masomo yao na kuongeza uelewa kuhusu mchango wa bandari katika uchumi wa taifa.

Wameongeza kuwa Bandari ya Dar es Salaam ina manufaa na tija kubwa kwa taifa kutokana na nafasi yake katika kurahisisha biashara na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button