Tanzania , Malawi kujizatiti uwekezaji

DAR ES SALAAM: Tanzania na Malawi zimekubaliana kuongeza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili kwa kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi, kuongeza thamani ya malighafi na kutumia fursa za masoko ya kikanda, huku Malawi ikiendelea kuitumia Tanzania kama lango muhimu la biashara kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Makubaliano hayo yamejadiliwa katika mkutano wa biashara na uwekezaji uliofanyika Dar es Salaam Septemba 7, 2026, na unaotarajiwa kufanyika kwa siku tatu, ukiwakutanisha wadau wa biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Malawi.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii wa Malawi, Itaye Simon, amesema nchi hizo zina fursa kubwa ya kushirikiana katika mnyororo wa thamani, ambapo Malawi inaweza kuzalisha malighafi kama soya, huku Tanzania ikiongeza thamani kupitia viwanda na bidhaa hizo kurejea katika masoko ya nchi hizo mbili.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, amesema Tanzania ina fursa ya kuongeza mauzo ya bidhaa katika soko la Malawi kwa takribani dola milioni sita za Marekani.

Amesema bidhaa zenye fursa katika soko hilo ni pamoja na samani, vifaa vya usafi, vigae, bidhaa za ujenzi, mbegu za mboga, sabuni na bidhaa za chuma.

Londo amezitaka Serikali na wafanyabiashara kutumia fursa hizo kuongeza biashara na manufaa kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Mkurugenzi wa TANTRADE, Ephraim Mafuru, amesema mwaka uliopita Tanzania ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 86 kwenda Malawi, akiwataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kukutana na wanunuzi na kuongeza mauzo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji Uwekezaji kutoka TISEZA, George Mkono, amesema Tanzania inalenga kuwavutia wawekezaji kutoka Malawi kuwekeza nchini, hususan katika kuongeza thamani ya malighafi zinazozalishwa Malawi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button