‘Huduma za afya zisogezwe kwa wananchi’

KIGOMA: Halmashauri za Mkoa wa Kigoma zimetakiwa kuipa kipaumbele miradi ya sekta ya afya ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kwa gharama nafuu.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Wazo Mwang’onda, alisema hayo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu wakati mwenge wa uhuru ukiweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Kituo cha afya cha Vitoliany kinachomilikiwa na mtu binafsi.

Mwang’onda alisema afya ni kipaumbele kwani inagusa maisha ya kila siku na kwamba serikali imedhamiria kuona huduma za afya zikipatikana karibu na makazi ya wananchi kwa gharama nafuu kupitia afya kwa wote hivyo halmashauri lazima zitekeleze kwa vitendo dhamira hiyo ya serikali.

Sambamba na hilo akiweka jiwe la msingi katika kituo hicho cha Vitoliany amepongeza watu binafsi wanaounga mkono serikali katika utoaji huduma za afya ambapo amezitaka halmashauri kuwasaidia wawekezaji binafsi kuhakikisha uwekezaji wao unafanikiwa na miradi iweze kusaidia utoaji huduma kwa jamii.

Awali, Mkurugenzi wa kituo hicho cha afya cha Vitoliany, Dk. Wellyngton Kabadi alisema kuwa hadi kukamilika kituo hicho kitagharimu kiasi cha Sh Bilioni 1.5 ikiwa ni mapato ya ndani ya taasisi hiyo ni mikopo kutoka taasisi za fedha na hadi sasa kiasi cha Sh milioni 900.5 zinetumika mradi ukifikia asilimia 70 ya utekelezaji.

Dk.Kabadi ambaye ni daktari bingwa wa macho alisema kuwa mradi utakapokamilika mwaka 2028 utatoa huduma jumuishi za uzazi salama ikiwemo kufanya upasuaji, matibabu ya macho ya kibingwa na huduma nyingine za matibabu hivyo wananchi kupata huduma hizo karibu na maeneo yao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button