Vijana waliopata ufadhili wa masomo wawasili N-AIST

ARUSHA; Vijana waliopata ufadhili wa mafunzo kupitia Programu ya Samia Scholarship Extended, wamewasili Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia Nelson Mandela (NM-AIST), jijini Arusha kuanza mafunzo hayo ya miezi 10 leo Septemba 14,2026.

Vijana hao ni sehemu ya kundi la pili la programu hiyo, ambapo 50 wameanza mafunzo ya miezi 10 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia Nelson Mandela (NM-AIST), jijini Arusha, huku 10 wengine wakitarajiwa kwenda nchini Urusi kwa mafunzo ya lugha kabla ya kuendelea na masomo yao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kundi hilo jijini Arusha, Mratibu wa Samia Scholarship Extended, Profesa Lilian Pasape, alisema wanafunzi 50 waliopokelewa NM-AIST ni 41 wavulana na tisa wasichana, ambapo 25 wanatoka shule za serikali na 25 za binafsi.

Alisema wanafunzi hao wametoka mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Tanga, Singida na Dodoma, jambo linaloonesha kuwa fursa hiyo imewafikia vijana kutoka maeneo mbalimbali.

Profesa Pasape alisema katika kipindi cha miezi 10, vijana hao wataandaliwa kitaaluma na kimaisha, ikiwa ni pamoja na kupatiwa bima za afya, hati za kusafiria na maandalizi ya kufanya mitihani ya kimataifa itakayowawezesha kuomba nafasi katika vyuo mbalimbali.

Profesa Pasape alisema baadhi ya wanufaika wa kundi lililopita tayari wameibua bunifu ambazo zimesajiliwa, huku NM-AIST ikishirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutafuta namna ya kuzifanyia kazi na kuzifikisha katika matumizi ya jamii.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button