Masauni atoa wito kulinda tabaka la Ozoni

DAR ES SALAAM: SERIKALI imewataka Watanzania kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku pamoja na vifaa vinavyotumia gesi zinazoharibu Tabaka la Ozoni, ikiwemo majokofu na viyoyozi vilivyotumika, ili kulinda mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, katika tamko lake kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni, yanayoadhimishwa Septemba 16 kila mwaka.

Masauni amesema Tabaka la Ozoni lina umuhimu mkubwa katika kulinda dunia kwa kuchuja sehemu kubwa ya mionzi hatari ya jua kabla haijafika kwenye uso wa dunia.

Amesema uharibifu wa tabaka hilo unaweza kuongeza kiwango cha mionzi ya jua kinachofika duniani na kusababisha madhara mbalimbali kwa afya za binadamu na mazingira, ikiwemo saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, kudhoofika kwa kinga ya mwili na kuzeeka kwa ngozi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, uharibifu wa Tabaka la Ozoni unaweza pia kuathiri ukuaji wa mimea, kuongeza joto duniani na kuchangia mabadiliko ya tabianchi.

Masauni amesema shughuli mbalimbali za kibinadamu zinachangia kuharibu Tabaka la Ozoni, hasa matumizi ya kemikali zinazotumika katika majokofu na viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji wa chuma, utengenezaji wa magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku, kilimo cha maua na uhifadhi wa nafaka maghalani.

Amesema Tanzania itaungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni, ambayo huadhimishwa kila Septemba 16 ikiwa ni kumbukumbu ya kutiwa saini kwa Itifaki ya Montreal ya mwaka 1987 kuhusu kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni.

Masauni amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inalenga kuhimiza hatua za kimataifa za kulinda Tabaka la Ozoni na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku ikitambua miaka 10 tangu kupitishwa kwa Marekebisho ya Kigali mwaka 2016.

Amesema utekelezaji wa marekebisho hayo unaonesha namna ambavyo dunia inaweza kuungana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za mazingira.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imepanga kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi Tabaka la Ozoni na kuhamasisha matumizi ya kemikali rafiki kwa mazingira.

Aidha, Serikali itatoa mafunzo kwa maafisa forodha na wasimamizi wa sheria kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kupitia Bandari Kuu ya Dar es Salaam, pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Masauni amewataka wananchi kununua bidhaa zenye nembo rasmi zinazoonesha kuwa ni “Ozone friendly” au zenye “low global warming potential”, yaani bidhaa rafiki kwa Tabaka la Ozoni au zenye uwezo mdogo wa kuchangia ongezeko la joto duniani.

Pia amewataka wananchi kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani na vifaa vya kuzimia moto vyenye kemikali zinazoweza kuharibu Tabaka la Ozoni au kuchangia ongezeko la joto duniani.

Amesema ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinafanikiwa.

Masauni amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika juhudi za kulinda Tabaka la Ozoni, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa sasa ni muhimu kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button