Balozi Mbarouk awasilisha hati za utambulisho Serbia

SERBIA: BALOZI wa Tanzania, Jamhuri ya Serbia, Mbarouk Nassor Mbarouk, amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Serbia, Aleksandar Vučić, katika Ikulu ya nchi hiyo iliyopo jijini Belgrade.

Uwasilishaji wa hati hizo unaashiria kuanza rasmi kwa Balozi Mbarouk kutekeleza majukumu yake ya kidiplomasia nchini Serbia na kuthibitisha dhamira ya Tanzania ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Baada ya kuwasilisha hati hizo, Balozi Mbarouk aliwasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa Rais Vučić, Serikali na wananchi wa Serbia.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Mbarouk aliainisha vipaumbele vya kipindi chake cha uwakilishi, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Serbia katika maeneo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Alisema mkazo utawekwa katika kuongeza ushirikiano katika sekta muhimu zikiwemo biashara, kilimo, uwekezaji na elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya uhusiano wa kihistoria wa urafiki uliopo kati ya mataifa hayo mawili.

Aidha, Balozi Mbarouk alieleza dhamira ya kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Serbia, taasisi za nchi hiyo, jumuiya ya kidiplomasia pamoja na sekta binafsi ili kutekeleza vipaumbele hivyo na kubaini fursa mpya za ushirikiano.

Kwa upande wake, Rais Vučić alimkaribisha Balozi Mbarouk na kumpongeza kwa kuteuliwa kwake, huku akimtaka kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio na kumuahidi ushirikiano wakati wowote atakapohitaji.

Pande hizo mbili pia zilithibitisha dhamira ya kuimarisha mazungumzo ya kisiasa katika ngazi ya juu pamoja na kubaini fursa mpya za kuanzisha mipango ya pamoja ya kiuchumi.

Balozi Mbarouk ni Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Italia na pia ana ithibati ya uwakilishi usio wa ukaazi katika mataifa kadhaa na mashirika ya kimataifa, akitekeleza majukumu yake kutoka Ubalozi wa Tanzania mjini Roma.

Jamhuri ya Serbia ni miongoni mwa Jamhuri sita zilizokuwa zikiunda iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia kabla ya kuvunjika mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button