KIBIti yajiweka tayari ukabili El-Nino

PWANI: SERIKALI ya Wilaya ya Kibiti imeweka mikakati ya kukabiliana na mvua za El Nino, ikiwemo kuwaandalia maeneo ya muda wanafunzi wa shule 12 za msingi ambazo zimekuwa zikikumbwa na mafuriko mara kadhaa.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo, alisema hayo jana wakati akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wilayani humo kuhusu namna walivyojiandaa kukabiliana na mvua hizo, ambazo zimetabiriwa kuanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi Oktoba.
Alisema kata nane zipo katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko, huku kata tano zikiwa katika hatari kubwa zaidi, hivyo Serikali imebaini shule zinazoweza kuathirika na tayari imeweka mpango wa kuwaandalia wanafunzi maeneo ya kukaa kama kambi, chakula, vifaa vya matumizi pamoja na vifaa vya uokoaji, ikiwemo boti.
“Pamoja na shughuli za usafi wa mitaro kuendelea kufanyika, ni wazi wananchi wanatakiwa kulitambua hili na kuchukua tahadhari, japo tayari tumekwishaandaa makambi, ikiwemo eneo la Nyamisati na shule ya msingi Kitundu,” alisema Kolombo
Kanali Kolombo aliwataka wananchi wa Wilaya ya Kibiti, hasa wanaofanya shughuli za uvuvi na wale wanaoishi mabondeni, kuchukua tahadhari kutokana na mvua hizo zilizotabiriwa.
Alisema zaidi ya kaya 3,000 zilizopo katika maeneo ya delta yanayojumuisha kata za Kiongoloni, Msala, Mbuchi, Salale na Mtunda zinaendelea na shughuli za kilimo na uvuvi, hivyo ni lazima zichukue tahadhari kwa ajili ya usalama wa familia zao.
“Najua hayo ndiyo makazi yao kwa sababu wengi wamezaliwa huko, wamesoma huko na kukulia huko, lakini mvua zilizotabiriwa safari hii ni nyingi kuliko za mwaka 2024. Hivyo, natoa wito kila mtu kuondoka mabondeni,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi wanaoishi kandokando ya Mto Rufiji kuendelea kuchukua tahadhari kwa kusogea maeneo ya juu kulingana na hali ya maji na mwenendo wa mvua.



