MsingiTek kunufaisha zaidi ya wanafunzi 13,000 Shinyanga

SHINYANGA: Kiwango cha kujua stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kinatarajiwa kuongezeka huko Shinyanga baada ya kuzinduliwa rasmi wa mpango shirikishi wa ujifunzaji kwa kutumia vishikwambi (MsingiTEK) uliolenga kuwafikia zaidi ya wanafunzi 13,000 wa shule za msingi 100 mkoani humo.
Mpango huo umezinduliwa na ofisa elimu mkoa, Samson Hango Septemba 17, 2026 mjini Shinyanga na kushuhudiwa na viongozi wa mbalimbali wa serikali wakiwemo wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi watendaji wa halmashauri, maafisa elimu wilaya za Shinyanga DC na Kishapu, walimu na wawakilishi wa wanafunzi wanaotarajiwa kunufaika na programu hiyo kabambe.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa MsingiTek, ofisa elimu mkoa wa Shinyanga aliwatala viongozi mbalimbali wa elimu kuimiliki na kuitekeleza kwa dhati na mradi huo ili uwe endelevu.
“Nina uhakika kuna wanafunzi wamealikwa kwenye hafla hii ila shuleni kwao hawajawai kutumia vishwambi, hivyo nafikiri ni jambo zuri tukajiongeza kama halmashauri, kuendeleza mkakati wa Dr Samia Suluhu Hassan wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia digitali ya sasa,“ Hango alisema.
Naye, Cliodhna Ryan, mkurugenzi wa programuwa Shirika la Imagine Worldwide, alisema kupitia kupitia ushirikiano mkubwa wa ndani yaani Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, jumla ya shule 50 zimefikiwa huku mpango huo ukilenga kufikia zaidi ya wanafunzi 13,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Aidha, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, mpango huo unatarajiwa kuzifikia jumla ya shule za msingi 100 ndani ya mkoa wa Shinyanga pekee.
Kwa mujibu wa Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Nguzo Mbili, Jafari Kasanga, awali utoro ulikua ni tatizo kuu shuleni, lakini sasa hivi watoto wanahudhuria shuleni kwa wingi na wanafaulu vizuri.
SOMA: Helios yazindua maabara ya Tehama, wanafunzi 873 Kalenga kunufaika
“Kabla ya mradi huu mahudurio ya wanafunzi yalikua ni asilimia 70 mpaka 75 ila kwa sasa mahudhurio si chini ya asilimia 95 kila siku. Watoto wanapenda sana kijifunza kupitia vishkwambi,” aliongeza.
Candy Allan John, mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Maganzo alisema kuwa kishwambi kimenisaidia kujifunza namna ya kujibu maswali ya mafumbo na kuhesabu, hali iliyoinua uwezo wake wa kusoma, kuandika na kuhesabu.
MsingiTek ni mpango unatekelezwa kupitia ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, pamoja na shirika la Imagine Worldwide Tanzania.
Mpango huu unaunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha ujifunzaji wa msingi kwa kuwapatia wanafunzi wa darasa la 1–3 fursa ya kutumia teknolojia ya kujifunzia inayoendana na uwezo wa mtoto na kuakisi mtaala, huku ukiimarisha mifumo na uwezo unaohitajika kutoa elimu bora kwa kiwango kikubwa.
Uzinduzi huu unaashiria dhamira ya MsingiTek kuonea mkoani Shinyanga ambapo kwa sasa, shule 50 zinazoshiriki mpango huo ikiwa lengo ni kufikia jumla ya shule 100 ifikapo mwishoni mwa 2026.

Kwa sasa mpango huo unatekelezwa katika wilaya za Shinyanga na Kishapu ambapo zaidi ya wanafunzi 13,000 na walimu walimu 270 wanatarajiwa kunufaika.
Hadi Juni 2026, tayari MSINGITEK ilikuwa imezifikia shule za msingi za serikali 250 katika mikoa mitano ya Morogoro, Ruvuma, Tabora, Shinyanga na Manyara) na wilaya 11 na kuwanufaisha wanafunzi zaidi ya 57,000.
Mpango huu unatarajiwa kuendelea na kufikia shule 500 zitakazohudumia zaidi ya wanafunzi 120,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026 na unatarajiwa kusaidia kujenga uzoefu na ushahidi utakaoongoza utekelezaji wa siku zijazo.
MsingiTek ni mpango shirikishi unaounga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kuboresha stadi za msingi za Kusoma, Kuandika, na Kuhesabu (KKK).
Mpango huu unajumuisha programu ya kujifunzia inayoendana na uwezo wa mwanafunzi na kuakisi mtaala, vishikwambi (tablets) vinavyotumia nishati ya jua, na usaidizi kwa walimu ili kuwasaidia watoto kujenga stadi imara za kusoma na kuhesabu, huku ukiimarisha mifumo ya elimu na uwezo wa utekelezaji katika shule za serikali.



