“Imarisheni uhusiano, kusikiliza matatizo ya walimu”
MIGOGORO, kuhujumiana na kupunguza ari ya utendaji kazi katika maeneo ya kazi, husababisha utoaji wa huduma kuwa chini ya kiwango.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba amesema hayo katika kikao kazi na maofisa elimu, wakuu wa shule na waratibu wa elimu Kata, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo.
Komba amewaeleza kuwa wakiwa kama viongozi katika Shule zao wanapaswa kufanya vikao vya mara kwa mara ili kusikiliza na kutatua kero za walimu pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa masuala ya uendeshaji wa Shule.
Hiyo imetokana na ukweli kuwa walimu wote wana haki ya kujua kinachofanyika shuleni lakini pia kukumbushwa wajibu wao.
” Imarisheni mahusiano, jengeni utamaduni wa kusikiliza matatizo ya walimu wenu na kuyatatua, na kuwashirikisha mambo yote yanayoendelea shuleni, hii itapunguza manung’uniko na Malalamiko kwa walimu,” amesema.
Pia amewaagiza walimu wakuu na wakuu wa shule kuacha mara moja uchangishaji wa michango isiyo na kibali katika Shule zao mpaka pale mwongozo wa kiwilaya utakapotangazwa rasmi kwa kuwa imekuwa kero kubwa kwa wazazi na walezi.
Pia amewataka Waratibu Elimu Kata kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia miongozo ya Serikali katika utoaji wa elimu, wakihakikisha michango isiyo na kibali wala tija kwa wananchi inaachwa mara moja.
Manispaa ya Ubungo ina jumla ya wanafunzi 147,186 kati yao wanafunzi 105,983 ni wa Shule za Msingi na wanafunzia 41,203 ni wa Shule za sekondari.



