Nyumba za wageni zabanwa taarifa binafsi

TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imesema si takwa la kisheria mteja kuandika taarifa binafsi kwenye nyumba za kulala wageni.

Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji wa PDPC, Stephen Wangwe ametaja taarifa hizo kuwa ni pamoja na kuhusu mteja anakotoka, anakokwenda na kabila lake.

Wangwe alisema hayo mjini Morogoro juzi wakati akiwasilisha mada kwenye warsha ya dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa Jukwaa la Wahariri wa Vyombo vya habari Tanzania (TEF).

Alisema ni muhimu watu wakaifahamu sheria ili kuepuka kuingia kwenye matatizo na kwamba kuandika mtu anakotoka na kwenda au kabila lake havihusiani na yeye kufikia kwenye nyumba aliyokwenda kulala.

“Unakwenda nyumba ya kulala wageni unaambiwa andika ulikotoka na unakokwenda, kabila lako lakini haya yote ni taarifa binafsi na wanavunja sheria,” alisema Wangwe.

Aliongeza: “Au kipindi cha nyuma matokeo ya mitihani yalikuwa yanatangazwa kwa majina, inatakiwa kuweka namba ili kulinda taarifa za mtu.”

Kwa mujibu wa PDPC, ni muhimu kwa wamiliki wa nyumba za kulala wageni na taasisi nyinginezo kuzingatia sheria hiyo ili kuepuka kuvunja haki za faragha za watu.

Wangwe alisema tangu kuwepo kwa sheria hiyo mtu anapoona taarifa zake zimetumika bila ridhaa yake anaruhusiwa kulalamika ili hatua zichukuliwe.

“Taarifa zako zikitumika vibaya na huna kokote pa kulalamika maana yake hutakuwa na imani na huduma husika, kutokana na hali hiyo wapo ambao hawatoi fedha kwenye ATM hadi aende ndani ya benki, na kwamba baadhi ni kwa sababu wameshaumizwa kwa taarifa zao binafsi kuwa hadharani,” alisema.

Wangwe alisema sheria hiyo imekuwepo ili kurudisha imani kwa watu wote wanaochakata taarifa binafsi wanasajiliwa, kusikiliza, usuluhishi hadi mtu atakapopata haki yake.

Alisema misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi ni mkusanyaji au mchakataji akusanye kihalali, afanye kwa haki bila kuonea, afanye kwa uwazi na madhumuni mahususi bila kuvuka mpaka wake.

Katika sehemu ya hotuba ya kufunga warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu PDPC, Dk Emmanuel Mkilia alisema wakati wa uzinduzi wa tume hiyo Aprili 3, 2024, Rais Dk Samia Suluhu Hassan aliweka bayana dhamira ya serikali ya kuhakikisha haki ya faragha inalindwa kwa mujibu wa sheria.

Dk Mkilia alisema Rais Samia alisisitiza ushirikiano wa wadau wote vikiwemo vyombo vya habari ili kutekeleza sheria hiyo kwa ufanisi.

“Nichukue fursa hii kuwaomba wahariri na wanahabari wote nchini kuendelea kushirikiana nasi kwa karibu ili kutekeleza jukumu hili kwa maslahi mapana ya taifa letu,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button