Achagiza uvishaji mifugo hereni za kielektroniki

OFISA Mifugo wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Msafiri Mkunda, ametaka wafugaji kuchangamkia uvishaji wa hereni za kielektroniki mifugo yao ili itambulike kimataifa.

Utaratibu huo unaanza Novemba Mosi mwaka huu.

Aidha, mifugo isiyo na hereni haitaruhusiwa ndani ya minada ya Halmashauri ya Kongwa.

Akizungumza na wafugaji, Mkunda alisema wafugaji wanatakiwa kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwatafutia masoko kwa kuweka alama kwenye mifugo yao.

Alisema katika soko la kimataifa kwa kutumia alama iliyochapishwa kwenye hereni iliyovishwa, mdau wa mifugo anaweza kutambua nchi, mkoa na wilaya na hata kata ambapo mifugo inatokea.

Alisema kuwa hereni hizo za kielektroniki zinasaidia usalama wa mifugo kwa kuzuia wizi na kudhibiti kuenea kwa magonjwa, pia kuwawezesha kuikatia bima mifugo yao kwa ajili ya kudai fidia pindi mifugo inapokumbwa na majanga.

Kwa mujibu wa Mkunda, kuvisha hereni kulipangwa kuanzia Aprili, mwaka huu na kukamilika ifikapo mwisho wa mwezi huu na baada ya hapo mfugaji ambaye mifugo yake haitakuwa imevishwa hereni hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Alisema mfugaji anaweza kutozwa faini isiyozidi Sh milioni mbili kifungo cha miezi sita hadi mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

“Kuanzia Novemba mosi mwaka huu kwa utaratibu ambao tumejiwekea kwa wilaya yetu, mfugaji huyo hataruhusiwa kabisa kuuza mifugo yake ndani ya minada yetu rasmi,” alisema.

Alisema wakati lengo la wilaya ni kuvisha hereni mifugo ipatayo 165,379 ikihusisha ng’ombe, mbuzi, kondoo mpaka sasa jumla ya mifugo 14,386 imevishwa hereni.

Kwa upande wake, Isack Mwamba ambaye ni bwana mifugo wa kujitolea alitaja changamoto wanazokabiliana nazo katika kazi kuwa elimu ndogo kwa wafugaji juu ya hereni. Pia hakuna kifaa kama banio kuwashika mifugo wakati wa kuvisha hereni hivyo wanatumia nguvu na muda mwingi kukamata mfugo mmoja.

Kwa upande mwingine, Daud Masoud ambaye ni mfugaji wa Kata ya Kongwa, ameiomba serikali kupunguza gharama ili kuwawezesha kumudu gharama za utaratibu huo, malisho na dawa kwa ajili ya mifugo yao.

Uvishaji wa hereni za kielektroniki ni mwendelezo wa jitihada za serikali za tangu mwaka 2015 ambapo serikali iliagiza utiaji chapa kwa mifugo kwa njia za asili, sasa teknolojia mpya ya hereni inahamasishwa kwani mifugo inaweza kutambulika kirahisi mahali inapotokea ikihusisha nchi, mkoa, wilaya na kata.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button