AFDP yawainua wavuvi na wafanyabiashara Kipumbwi

PANGANI, TANGA: Wananchi wa Kata ya Kipumbwi, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, wameeleza kunufaika na Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.

Hayo yameelezwa Septemba 8, 2026, na wawakilishi wa wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi kutoka Kata ya Kipumbwi wakati wa ziara ya Timu ya IFAD ya kutathmini utekelezaji wa programu hiyo katika mapitio ya utekelezaji wa kipindi cha kati (MTR).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu wa Umoja wa Wachakataji Dagaa Kipumbwi (UWADAKI), Abdallah Mohamed, amesema AFDP imelenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuongeza kipato na uzalishaji wa mazao ya uvuvi, kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa, kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi, kuboresha lishe pamoja na kuzingatia masuala ya jinsia.

Amesema kupitia programu hiyo, makundi mbalimbali yamenufaika, yakiwemo Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU), vyama vya wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara wadogo wa mazao ya uvuvi.

Kwa mujibu wa Mohamed, AFDP pia imewezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayolenga kuboresha shughuli za uvuvi na biashara ya mazao ya uvuvi, ikiwemo soko la kimataifa la samaki, vichanja vya kukaushia dagaa, mtambo wa kuzalisha barafu na chumba cha ubaridi.

Amesema miundombinu hiyo inatarajiwa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa, kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza thamani ya mazao na upatikanaji wa masoko, huku ikichochea usalama wa chakula na lishe pamoja na kuongeza fursa za ajira.

Aidha, Mohamed amesema wananchi wamepatiwa mafunzo mbalimbali, yakiwemo elimu ya fedha na ujasiriamali, yaliyolenga kuwasaidia wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara wadogo kuanzisha na kuendesha biashara zenye mafanikio pamoja na kusimamia vizuri mapato na matumizi.

Amesema mafunzo ya lishe yamelenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa watoto na makundi mbalimbali kulingana na umri, pamoja na uhusiano kati ya lishe bora, afya na uwezo wa kufanya kazi.

Kwa upande mwingine, mafunzo ya jinsia yamelenga kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za kiuchumi na katika maamuzi ya familia na vikundi, sambamba na kuwezesha usawa wa fursa katika uzalishaji, biashara na matumizi ya mapato.

Vilevile, AFDP inalenga kuchochea uvuvi endelevu unaozingatia mabadiliko ya tabianchi na kuongeza upatikanaji wa samaki, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato cha wananchi katika ngazi ya jamii na Wilaya ya Pangani kwa ujumla.

Katika ziara hiyo, wataalamu waliendelea kuhamasisha ushirikishwaji wa makundi yote katika jamii kwa usawa, kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa mazao ya uvuvi na kuweka mifumo na mipango madhubuti ya kuhakikisha uendeshaji endelevu wa soko hilo la kimataifa la samaki.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha soko hilo linatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Kipumbwi, Pangani na Taifa kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button