Ajali ya daladala yaua 4, yajeruhi 46

PWANI; Basi la abiria ‘daladala’ limepinduka eneoo la Kona ya Kinyanyiko, Barabara ya Pugu-Kisarawe, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani na kusababisha vifo vya watu wanne, huku 46 wakijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase amesema ajali hiyo ilitokea Agosti 9 mwaka huu majira ya saa 11 jioni na kuwataja waliokufa ni dereva wa gari hilo Salehe Mtumwa (35), Mwika Gwesele (38), Fatuma Momba na Sivijui Samatha (40), wote wakazi wa Dar es Salaam.
Amesema kuwa majeruhi wengine 29 walipatiwa matibabu Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe na kuruhusiwa, huku majeruhi 10 wakiendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili na majeruhi wengine saba wanaendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe.
Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa daladala hilo, ambapo dereva alishindwa kulimudu kwenye mteremko mkali, hivyo kusababisha kupinduka.



