Ajira 1,000 zaja Zimamoto na Uokoaji

SERIKALI imetenga ajira mpya 1,000 kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambazo zitatolewa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi alisema hayo mjini Morogoro jana akifungua kikao cha baraza dogo la wafanyakazi wa jeshi hilo.

Mkomi alisema ofisi hiyo inaendelea kufanya jitihada kuhakikisha uboreshaji unafanyika kiutendaji hususani katika upatikanaji wa askari wapya.

“Kama ambavyo imeelezwa, tumetoa kibali cha watumishi wapya 425 na pia kwenye bajeti inayokuja (2025/2026), tumetenga watumishi wapya 1,000 na tunaangalia ukubwa wa majukumu tuliyokuwa na changamoto zilizoelezwa, nahisi hata hawa 1,000 hawatatosha,” alisema.

Mkomi alisema kuna ujenzi wa vituo vipya saba vya Zimamoto na Ukoaji na miradi ya kimkakati ambayo ni Kiwanja cha Ndege Msalato ambacho kinahitaji watumishi 164 wa jeshi hilo.

Alitaja mradi mwingine ni ujenzi wa kiwanja cha ndege mkoani Shinyanga ambacho kinahitaji watumishi 78 wa jeshi hilo. Vilevile kiwanja cha ndege Mtwara ambacho kimekamilika na kina watumishi wachache wa jeshi hilo.

Uongozi wa jeshi hilo ulisema kwa sasa wanahitajika watumishi 7,552.

“Maana yake, bado mahitaji ya watumishi ni kubwa zaidi na kila tunavyosonga mbele, mahitaji yanaongezeka,” alisema Mkomi.

Aliongeza: “Nimeambiwa kwenye SGR ambapo tumeanzia Dar es Salaam- Morogoro hadi Doodma , tunahitaji watumishi lakini mradi huo unaenda mbele zaidi na tutahitaji watumishi wengi zaidi.”

Alisema serikali kwa mwaka huu wa fedha imetenga watumishi wapya 425 na kibali lilichatolewa na jeshi hilo, kipo kwenye hatua za mchakato wa kuwapata na kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026 imetenga watumishi wapya 1,000.

Katibu mkuu pia alilitaka jeshi hilo wakati wa kufanya usaili wa kupata askari wapya, lifuate sheria, kanuni na utaratibu pasipokuweka upendeleo ili kuwapata askari wenye uwezo ndani ya jeshi hilo.

Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Masunga alisema jeshi hilo linaendelea kuomba vibali vya ajira kila mwaka kutoka katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kukabili upungufu wa rasilimaliwatu.

“Kwa mwaka 2024/2025, jeshi limepata kibali cha ajira kwa askari wapya 425 na taratibu za kuajiri askari hao zinaendelea,” alisema Masunga.

Alisema jeshi hilo limepokea Sh bilioni 2.6 kwa ajili ya kumalizia vituo saba vya zimamoto na uokoaji katika mikoa ya Simiyu, Kagera, Geita, Songwe, Katavi, Njombe na Manyara.

Pia, alisema Jeshi hilo limepokea Sh milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha Mkoa wa Morogoro.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button