Wanawake watakiwa kuwa mstari wa mbele malezi ya watoto

MOROGORO: MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Sheila Lukuba, amewasihi wanawake kuwa mstari wa mbele katika malezi ya watoto kwa kuwajenga katika misingi ya uzalendo ili watambue kuwa hawana nchi nyingine isipokuwa Tanzania.

Lukuba ameyasema hayo katika sherehe za Siku ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) zilizofanyika katika Parokia ya Mt. Fransisco wa Sales, Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro.

Amesema ni wajibu wa wanawake kurejesha nguvu katika malezi ya watoto na vijana ili kujenga taifa lenye watu shupavu, wenye misimamo inayojenga uzalendo na kudumisha amani ya nchi.

“Nimefurahishwa namna risala yetu mlivyogusia suala la malezi ya watoto. Ndugu zangu kina mama, Kanisa linaweza kumfundisha mtoto kwa saa moja au mbili, isipokuwa familia ndiyo inayomfundisha mtoto kwa maisha yake yote,” amesema Lukuba.

Amesema watoto wanahitaji kuona imani ikimulika kupitia matendo ya wazazi wao ya kila siku nyumbani, ikiwemo kuwaona wakisali, wakiheshimiana, wakizungumza kwa upendo na kushiriki katika maisha ya kawaida pamoja na shughuli za Kanisa.

Katika hatua nyingine, Lukuba ametoa Sh milioni moja kusaidia shughuli za Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Kata ya Lukobe, pamoja na vitabu 20 vyenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu changamoto zinazowakabili Wakatoliki.

Fedha hizo zilikabidhiwa kwa wanawake hao kupitia Diwani wa Viti Maalumu Manispaa ya Morogoro, Imakulata Mhagama, ambaye amesema mbunge huyo ataendelea kutafuta wadau mbalimbali watakaotoa msaada wa hali na mali ili kuwawezesha wanawake hao kukuza chama hicho.

Lukuba pia amewakumbusha wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuhusu taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwepo wa mvua za El Niño, akiwataka kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa.

Amesema wananchi wanapaswa, miongoni mwa mambo mengine, kuhama maeneo ya mabondeni, kusafisha mitaro na mito pamoja na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi.

“Niwaombe tusimame katika maombi ili Mungu aiepushe nchi yetu na gharika au atupe mvua za kiasi,” amesema Lukuba.

Kwa upande wake, Paroko wa Parokia hiyo, Padre Simoni Nabende, amesema mwanamke ambaye ni mama ni moyo wa familia na nguzo katika jamii, akieleza kuwa malezi bora yanasaidia kujenga misingi ya amani na kuandaa viongozi bora wa Kanisa pamoja na Taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button