Baba Arafat jela maisha ya kumnajisi mtoto

DAR ES SALAAM: MAHAKAMA ya Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, imemhukumu Salum Sume ,34, maarufu kwa jina la Baba Arafat, mkazi wa Mbagala kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka mitano.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Catherine Madili, amesema kuwa ushahidi uliowasilishwa na mashahidi wa upande wa mashtaka uliithibitishia mahakama kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo bila shaka yoyote.
Kesi hiyo ya jinai namba 2663/2024 ilimhusu Salum Sume, aliyeshtakiwa kwa kosa la ubakaji kinyume na vifungu 130 (1) (2) (e) na 131(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Rejeo la mwaka 2022. Kulingana na hati ya mashtaka, mtuhumiwa alitenda kosa hilo mwaka 2023 katika eneo la Juhudi, Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Sume alimbaka mtoto huyo mdogo, kitendo ambacho kimeelezwa kuwa cha kinyama na cha kikatili. Waendesha mashtaka waliomba mahakama kutoa adhabu kali ili kutuma ujumbe mkali kwa wahalifu wa makosa kama haya.
Baada ya kusikiliza ushahidi na kujiridhisha, Mahakama ilimkuta mtuhumiwa na hatia na kumpatia adhabu ya kifungo cha maisha jela. Hukumu hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wananchi, wengi wao wakieleza kuwa ni hatua muhimu katika kupambana na ukatili dhidi ya watoto.



