Barabara ya Ruangwa – Nanganga mambo safi

LINDI; UJENZI wa Barabara ya Nanganga hadi Ruangwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 53.2 umefikia asilimia 97.49.

Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi wameeleza furaha yao kuwa mradi huo utabadilisha maisha yao na kuwanufaisha kiuchumi.

Kwa mujibu wa mkandarasi, Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Cooperation (CR15G), kazi iliyobaki ni kuweka alama na michoro ya barabarani pamoja na kazi ya kusimika taa za barabarani ambayo inaendelea.

Mradi huo wa Barabara ya Ruangwa-Nanganga ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa Barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga yenye urefu wa kilometa 106 inayojengwa na CR15G kwa fedha za Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Ipo chini ya mshauri Kitengo cha Ushauri wa Uhandisi Tanroads (TECU). Ujenzi wa kipande cha Ruangwa-Nanganga ulianza Agosti 2020 na ulitarajiwa kutumia miezi 27 lakini uliongezewa muda na sasa unatarajiwa kukamilika Agosti 25 mwaka huu.

Una thamani ya Sh bilioni 58.6 bila VAT. Kwa mujibu wa taarifa ya mkandarasi katika eneo la mradi mwishoni mwa wiki, mradi huo unakamilisha kazi ya kuweka taa za barabarani ambazo zitakuwa 731 na zimeshasimikwa taa takribani 400.

HabariLEO ilishuhudia mafundi wakiendelea na kazi hiyo katika eneo la Kata ya Nkowe ambako diwani wa eneo hilo, Uwesu Ngonapala alikuwa miongoni mwa mashuhuda wa kazi inayoendelea. “Mwanzo wananchi hawakuwa wanaamini kama kweli taa za barabarani zitawekwa.

“Walipoona zimeanza kuwekwa, wakanipigia simu… diwani tumeona taa zimewekwa. Nikawaambia na nyingine zinaendelea kuwekwa,” alieleza.

Aliishukuru serikali na aliyekuwa mbunge wao, Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa kwa miradi ya maendeleo ukiwamo huo wa Barabara ya Ruangwa – Nanganga ambayo itakwenda hadi wilayani Nachingwea.

Mkazi wa Kijiji cha Michenga A, Hamis Bakari alieleza kuwa usafiri umerahisishwa kwenda Nanganga na Ruangwa na kuwekwa kwa taa kumesaidia kufanya shughuli zao za kujipatia riziki kando ya barabara hata nyakati za usiku na pia kwa akinamama wanaoenda kisimani. Kwa upande wake, Shabaan Lukanga aliomba taa zaidi kwenye eneo ambako kuna kisima ili kuwaepusha akinamama na hatari zikiwamo za wanyamapori wanaokatiza usiku eneo hilo.

Moja ya alama kubwa nyingine za mradi huo ni kujengwa kwa Daraja la Lukuledi ambalo lilikuwa eneo korofi na lililosababisha kukwama kwa mawasiliano wakati wa mvua na hivyo kuleta adha kwa wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button