Bodi ETDCO yaridhishwa mradi wa umeme Tabora -Katavi

BODI ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (ETDCO) imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi unaendelea na utaingia kwenye gridi ya taifa Juni mwaka huu.
Aidha, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi utaanza kupata umeme huo mwishoni mwa Juni mwaka huu na kuufanya mkoa huo kupata umeme wa uhakika na kuondokana na uhaba uliokuwepo.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Raymond Mbilinyi, amesema hayo wakati bodi hiyo ilipotembelea maendeleo ya mradi huo na kusema yanaridhisha na mwishoni mwa Juni mwaka huu mradi huo utakuwa umekamilika.
“Tumeridhishwa na maendeleo ya mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, utekelezaji wake umefika asilimia 96 na Juni mwishoni Mpanda itakuwa na umeme wa gridi,’amesema Mbilinyi.
Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Sadock Mugendi, amesema ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri na sasa upo hatua za mwisho za ukaguzi wa laini ya umeme.
Amesema hadi mwishoni mwa Juni, mradi utakuwa umekamilika kwaasilimia 100 na kwa kufikisha umeme huo mkoani Katavi hivyo kuufanya mkoa huo kuingia rasmi kwenye gridi ya taifa na kuondokana na adha za umeme.
Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania-Kanda ya Magharibi, Richard Swai, alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Tabora na Katavi.
Kutokana na hilo amewataka wananchi wa mikoa hiyo kujiandaa kupokea umeme wa gridi ya taifa, ambao utachochea shughuli za kiuchumi na maendeleo kupitia sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, usindikaji na uongezaji thamani wa mazao.