BoT yatoa mafunzo kubaini noti halali

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo ya kutambua noti halali kwa makundi maalumu wakiwamo wenye ulemavu.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Meneja Msaidizi Sarafu BoT, Joyce Saidimu alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwawezesha kupata uelewa wa kutosha wa kujua alama za usalama kwenye sarafu.

Alisema elimu waliyowapa itawawezesha kugundua fedha halali kwani ni makundi ambayo yamekuwa yakisahaulika katika masuala ya kijamii.

“Sisi kama BoT, ni utaratibu wetu kutoa mafunzo kama hayo shuleni, sokoni na kwenye maeneo mbalimbali ya biashara, ila kwa awamu hii tumeamua kutoa elimu kwa watu wa makundi maalumu ili waweze kupata uelewa wa kutosha na kutambua noti halali,” alisema.

Aliongeza: “Mafunzo haya yatakuwa endelevu na tutakuwa tukiyatoa mara kwa mara ili waweze kupata uelewa wa kutosha juu ya masuala haya na kuepuka kushikishwa fedha bandia kwani tayari wana uelewa wa kutosha.”

Aidha, BoT imetoa mafunzo ya namna sahihi ya kutunza fedha kwa ajili ya matumizi yao huku akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa kufundisha wenzao namna ya kutunza fedha.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Jamii na Viziwi (DCPO), Jafari Shabani alisema waliomba kupatiwa mafunzo hayo kwa watu wenye ulemavu kutokana na changamoto mbalimbali walizokuwa wakikabiliana nazo katika kutambua noti bandia na halali.

Alisema jumla ya watu wenye mahitaji maalumu 70 walipatiwa mafunzo hayo.

Jafari alisema watu hao wenye mahitaji maalumu walikuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo na hata kusababisha wengi wao kupelekwa katika vyombo vya usalama wanapokutwa na noti bandia kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya utambuzi wa alama za usalama kwenye sarafu.

Kwa upande wake, mshiriki wa semina, Emmanuel Benjamin aliishukuru Benki Kuu kwa mafunzo hayo.

Alisema aliwahi kupewa noti bandia katika biashara yake ya kuendesha bajaji na sasa baada ya kupatiwa elimu, ataweza kuchukua tahadhari mapema.

Aliomba mafunzo hayo kuwa endelevu huku akiomba serikali kutoa mafunzo zaidi kwa watu wenye ulemavu kwani ni hatua ya kundi hili kushirikishwa na kuondoa dhana ya kubaguliwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button