Boti yapiduka Ziwa Nyasa, Wakaa majini saa 6 kuokolewa

WATU saba wakiwemo raia wanne wa Uholanzi, wamenusurika kufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Bandari ya Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma kuelekea nchini Malawi kupata hitilafu Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.
Ajali hiyo ilitokea Julai 27, 2026 majira ya saa nne asubuhi, baada ya boti hiyo kupata hitilafu ya injini na kuanza kujaa maji kutokana na dhoruba kali na kisha kupinduka, kabla ya wasafiri hao kuokolewa saa 10 alasiri.
Akizungumza baada ya uokoaji kukamilika, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, aliwashukuru wananchi wa Wilaya ya Nyasa kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika uokoaji huo.
Amesema manusura wote wako salama na wanaendelea kupatiwa matibabu, huku akiwaomba wananchi kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika na kuepuka kusafiri ziwani wakati hali ya hewa si salama.
Mkuu huyo wa mkoa baada ya kutoka kwenye Bandari ya Mbamba Bay alienda kuwajulia hali hospitalini manusura hao ambao ni Hussein Hasa, Shadrack Mpata, Philemon Moyo, Hendrika Verveda, Christian Gerlagh, Lente Maarjse, Mitchel Haring.



