COPRA kuwaunganisha wadau kupitia Nanenane

Dodoma: Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imepanga kushiriki Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa 2026 yatakayofanyika kuanzia Agosti 1, 2026 kwenye viwanja vya Dk John Malecela, Dodoma, ikiwa na mpango maalumu wa kuwaunganisha wadau wa sekta ya nafaka na mazao mchanganyiko na fursa za masoko, biashara, teknolojia na uongezaji thamani.

Ushiriki wa COPRA unaendana na kaulimbiu ya Nanenane 2026, “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050,” kwa kuweka msisitizo katika uzalishaji unaozingatia mahitaji ya soko, ubora wa mazao, biashara rasmi, uongezaji thamani na matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija na ushindani wa mazao ya Tanzania.

Banda la COPRA litakuwa kitovu cha maarifa, huduma, biashara na ubunifu, ambapo wakulima, wafanyabiashara, wasindikaji, wawekezaji, vijana na wananchi kwa ujumla watapata elimu na ushauri wa kitaalamu kuhusu masoko ya ndani na kimataifa, viwango vya ubora, mifumo rasmi ya biashara, uongezaji thamani, teknolojia na huduma za kidijitali kupitia mfumo wa COPRAMIS.

Kipekee katika Nanenane 2026, COPRA itaandaa Warsha Maalumu ya Zao la Mahindi itakayofanyika tarehe 5 Agosti 2026. Warsha itakutanisha wadau kujadili uwekezaji kwenye uzalishaji, masoko, biashara, fedha na mitaji, uongezaji thamani na ushindani wa zao hilo. Aidha, Agosti 7, 2026, kutakuwa na siku ya watengeneza maudhui ya biashara ya mazao mtandaoni ‘Digital Agribusiness Influencers Day’, na kuwakutanisha na Mamlaka na kutoa fursa ya kupata ufahamu wa masoko na biashara rasmi ya nafaka na mazao mchanganyiko ili kuunganisha na kutumia nguvu ya mawasiliano katika kukuza taarifa za masoko, fursa za biashara, teknolojia na ubunifu.

Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Madeje Mlola, amesema ushiriki wa Mamlaka mwaka huu umejikita katika kuhakikisha wadau wanapata maarifa, taarifa sahihi, uelewa huduma na fursa zinazowawezesha kufanya maamuzi bora katika uzalishaji na biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button