MKUU wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewataka Wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27.
DC Mwenda ametoa rai hiyo September 5, 2024 wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Tulya, Migilango na Doromoni vilivyopo kata ya Tulya,tarafa ya Kisiriri, alipofanya Mkutano wa hadhara kwa lengo la kutoa maagizo mbalimbali ya Serikali.
“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa,niwaombe Wananchi tujitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa ajili ya kuwa wapiga kura kwenye uchaguzi huo pindi zoezi litakapoanza pia Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, linalotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu,’ amesema DC Mwenda.
DC Mwenda amewataka vijana kujjitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi. Aidha amesema kuwa ili mwananchi uweze kupiga kura huna budi kujiandikisha katika Daftari la Orodha ya Wapiga Kura.
“Ili uweze kupiga kura, lazima ujiandikishe katika daftari la orodha ya wapiga kura na zoezi la kujiandikisha litafanyika Octoba 11-20,2024 itakapofika tarehe hii, tujitokeze kwa wingi,” amesema DC Mwenda.
Katika hatua nyingine DC Mwenda amewataka vijana kujitokeza kwa Wingi kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi katika ngazi za vijiji na vitongoji ili waweze kuwa sehemu ya kutoa mchango wao katika maendeleo ya vijiji vyao