Fahamu miaka 90 ya mwanahabari Edgar Snow

BEIJING: Miaka 90 baada ya mwanahabari na mwandishi wa Marekani, Edgar Snow, kuandika kuhusu harakati za Chama cha Kikomunisti cha China, kazi yake imeendelea kuwa somo muhimu kwa wanahabari kuhusu umuhimu wa weledi, ujasiri na kuzingatia ukweli katika uandishi wa habari.

Snow, aliyeishi kati ya mwaka 1905 na 1972, alikwenda China mwaka 1936 na kuwa miongoni mwa wanahabari wa kwanza wa Marekani kuitambulisha harakati za Chama cha Kikomunisti cha China kwa nchi za Magharibi kupitia makala zake na kitabu chake maarufu Red Star Over China.

Katika kazi hiyo, Snow alifuatana na wapiganaji na wanaharakati wa Jeshi Jekundu wakati wa safari ya Long March, akifanya mahojiano, kupiga picha na kukusanya taarifa katika mazingira magumu ya kivita.

Licha ya changamoto hizo, kazi yake imeendelea kutajwa kama mfano wa uandishi wa habari uliozingatia uchunguzi na weledi, huku taarifa alizokusanya zikitoa picha ya harakati hizo kwa wasomaji waliokuwa nje ya China.

Akizungumzia umuhimu wa kumkumbuka Snow miaka 90 baadaye, mwandishi amesema historia yake inatoa somo muhimu katika kipindi ambacho sekta ya habari inakabiliwa na changamoto mpya, ikiwemo misukumo ya kisiasa na kifedha.

Amesema baadhi ya wanahabari wanaweza kushawishika kuandika habari zinazolenga kuvutia mapato au kuendeleza ajenda fulani za kisiasa, hali inayoweza kusababisha masuala muhimu kwa wananchi na taifa kutopatiwa uzito unaostahili.

Kwa mujibu wa mwandishi huyo, changamoto hiyo imekuwa muhimu zaidi katika zama za TEHAMA na Akili Mnemba, kutokana na kasi kubwa ambayo taarifa zinaweza kusambazwa na kuwafikia watu wengi.

Amesema hata pale mwanahabari anapokuwa hana nia mbaya, ukosefu wa weledi katika ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa taarifa unaweza kusababisha madhara kwa jamii na taifa.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia taasisi zake pamoja na mabaraza ya wanahabari zimekuwa zikifanya juhudi kuimarisha weledi katika sekta ya habari, lakini hatua hizo haziwezi kufanikiwa kikamilifu bila mwanahabari mwenyewe kuwa na dhamira ya kuzingatia ukweli na maslahi ya umma.

Amesisitiza kuwa weledi wa mwanahabari unaanzia kwa mtu mwenyewe, akitakiwa kujiuliza si tu kama taarifa anayoiandika ni ya kweli, bali pia athari ambazo kazi yake inaweza kuwa nazo kwa jamii na taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button