Huduma za anga zarejea Musoma

MUSOMA: Kurejea kwa huduma za usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) katika Kiwanja cha Ndege cha Musoma baada ya takribani miaka minane, kunatarajiwa kuongeza fursa za biashara, utalii na uwekezaji, huku wakazi wa Mkoa wa Mara na maeneo jirani wakipata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Safari hizo zitafanyika mara mbili kwa wiki, Alhamisi na Jumamosi, zikihusisha Dar es Salaam, Mwanza na Musoma, hatua inayotarajiwa kuimarisha uunganishaji wa Mkoa wa Mara na maeneo mengine ya Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati wa mapokezi ya ndege hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa, Gerald Kusaya, amesema kurejea kwa huduma hizo ni fursa muhimu kwa wananchi kutokana na mchango wa usafiri wa anga katika kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo pamoja na kukuza shughuli za biashara.
Kusaya amesema ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 78 na 80 itasaidia wakazi wa Mara na mikoa jirani kusafiri kwa urahisi zaidi, huku wafanyabiashara wakipata fursa ya kuunganisha masoko na maeneo mbalimbali kwa muda mfupi.

Ametoa shukrani kwa Rais Dk Samia kwa hatua za kuboresha na kupanua Kiwanja cha Ndege cha Musoma, pamoja na kulipa fidia wananchi waliokuwa wakiishi katika maeneo jirani na uwanja huo.
Kusaya amewataka wananchi kutumia huduma hiyo kwa wingi kwa kujaza ndege, akieleza kuwa matumizi makubwa ya huduma hiyo yatachangia katika kuhakikisha safari zinaendelea na hivyo kuongeza manufaa yake kwa uchumi wa mkoa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma, Frank Msofe, amesema safari ya mwisho ya ndege ya abiria ya Shirika la Precision Air katika kiwanja hicho ilikuwa Machi 2018.
Amesema kurejea kwa huduma za ndege ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Mara, huku akieleza kuwa mamlaka inaendelea kuimarisha miundombinu na kuhakikisha usalama wa abiria na ndege unaendelea kupewa kipaumbele.
Msofe amesema maboresho ya miundombinu yanaendelea kwa msaada wa Serikali ili kuhakikisha ndege zinatua na kuruka kwa usalama na kuongeza ufanisi wa huduma katika kiwanja hicho.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amesema kurejea kwa safari hizo kutafungua fursa kwa wafanyabiashara, wamiliki wa hoteli, wasafirishaji na wadau wa sekta ya utalii.
Amesema uwepo wa huduma za anga utaongeza mnyororo wa thamani katika shughuli za kiuchumi na kutoa mazingira zaidi ya wananchi kunufaika na biashara zinazohusiana na usafiri, utalii na uwekezaji.
Chikoka amesema huduma hiyo pia inaweza kuchochea uwekezaji katika hoteli za kisasa na za kitalii, hususan maeneo ya ufukweni, huku akieleza kuwa Serikali ina matarajio ya kushirikiana na mashirika mengine ya ndege ili kuongeza huduma za usafiri wa anga wilayani humo.
Aidha, amesema kiasi cha Sh milioni 34 kimetumika katika matengenezo ya kiwanja hicho, hatua inayotarajiwa kupunguza muda na gharama zinazotumiwa na wakazi wa eneo hilo kusafiri kwenda maeneo mengine kupata huduma za usafiri wa anga.
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji Kigera, amesema kurejea kwa usafiri wa anga kutarahisisha shughuli za wafanyabiashara, utalii na usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka.
Amewataka wananchi, hususan wafanyabiashara wa madini, samaki na dagaa, kutumia huduma hiyo kusafirisha bidhaa zao kwa ufanisi zaidi, kupanua masoko na kuongeza shughuli za kiuchumi.



