Jaji Werema kuzikwa Jumamosi Butiama

ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mstaafu Frederick Werema anatarajiwa kuzikwa Jumamosi ijayo kijijini kwao Kongoto, Wilaya ya Butiama mkoani Mara.
Akizungumza na HabariLEO jana nyumbani kwa Werema, Mikocheni mkoani Dar es Salaam, mdogo wake na Msemaji wa familia, Japhet Werema alisema leo mwili utatolewa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo na kupelekwa katika Kanisa Katoliki Mtakatifu Martha, Mikocheni.
“Baada ya ibada mwili uterejeshwa hapa nyumbani na tutaendelea na maombolezo,” alisema.
Alisema kesho itakuwa siku ya kuaga kwa taratibu zingine za kiserikali ambazo zinatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Karimjee.
Alisema baada ya kukamilika kwa taratibu za kiserikali, mwili utapelekwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambapo utalala hapo na Ijumaa usafirishwa kuelekea mkoani Mwanza na baadaye wilayani Butiama.
Japhet alisema maombolezo yataendela na Januari 4, Jaji Werema atazikwa katika Kijiji cha Kongoto, Butiama.
Werema ameacha mke, watoto watatu ambapo wa kiume wawili na wa kike mmoja na wajukuu watatu.
Alifariki dunia Desemba 30, mwaka jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alipokuwa akipatiwa matibabu.
Werema alizaliwa Oktoba 10, 1955 na amewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali, ikiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia 2009 hadi Desemba 16, 2014 alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Aliwahi pia, kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kitengo cha Biashara na alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mt Martha, Mikocheni, Jimbo Kuu Dar es Salaam.