Kamishna Mkuu Skauti amaliza muda wake

KAMISHNA Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania Grace Kado ametangaza kumaliza muda wake wa muhula wa kwanza wa uongozi uliodumu kwa miaka minne.

Kamishna huyo anaondoka wakati ambao chama hakina skauti mkuu baada ya kuwepo na mvutano wa uongozi kwa muda mrefu na kumuondoa aliyekuwa madarakani Mwamtumu Mahiza baada ya kumaliza muda wake.

Mgogoro huo ulihitimishwa na mkutano mkuu uliofanyika Julai 2 mwaka jana ambao ulipendekeza majina ya wanachama watatu ili mmoja wao ateuliwe kuwa skauti mkuu.
Kung’atuka kwa Grace kwenye nafasi hiyo ni kwa mujibu wa katiba ya chama hicho inayoelekeza kamisha mkuu kuachia nafasi pale anapomaliza muhula mmoja wa uongozi wake kabla ya kuteuliwa tena au kuteuliwa kwa kamishna mwingine.
Kulingana na katiba hiyo naibu kamishna  Abuu Mtitu ndiye atakayekaimu nafasi hiyo na kukiongoza chama hadi utakapokamilika
mchakato wa kumpata kamishna.
Akizungumza Makao Makuu ya Skauti Upanga jijini Dar es Salaam,  Grace amesema anaondoka kwenye nafasi hiyo akiamini kwamba chama kitaendelea kufuata misingi ya Katiba na miongozo ya sera.
“Chama bado kipo katika wakati ambao unahitaji zaidi mshikamano na hekima kubwa katika kutekeleza shughuli zetu. Niwapongeze skauti wote Tanzania kwa kuendelea kuonyesha ukomavu na busara.
“Tuendelee kutekeleza shughuli zetu kwa kufuata katiba bila kukiuka miongozo ya chama chetu, chama chetu kufiki ustawi wa miaka 100 ni jambo la kujivunia,”amesema Grace.
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa skauti Mtitu amesema anapokea kijiti hicho cha uongozi akiahidi kuendelea kuimarisha mshikamano na kuwataka wanachama kuiishi misingi ya skauti.

Habari Zifananazo

Back to top button