Kapinga ahimiza ulinzi wa mitaji, biashara zisaidiwe kukua

LINDI: WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amewataka watendaji wa serikali na taasisi za udhibiti kuwa wawezeshaji wa biashara badala ya kufungia biashara, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mitaji na maslahi ya wananchi.

Kapinga amesema hayo Agosti 10, 2026, wakati akizindua ghala la kuhifadhia mazao la Halmashauri ya Mji wa Masasi, lililopo Kata ya Mtandi lililo gharimu takribani Sh milioni 921.

“Ukikuta kiwanda hakina mifumo mizuri usikifungie, kisaidie kiweze kurudi kwenye ramani; ukikuta mtu hana leseni ya biashara, msaidie apate leseni badala ya kumfungia biashara,” amesema Kapinga.

Amesema mfanyabiashara anayekosa leseni asaidiwe kuipata, huku viwanda vyenye changamoto vikielekezwa kurekebisha kasoro badala ya kufungiwa, na ameagiza TBS kuwasaidia wajasiriamali wanaohitaji nembo na viwango vya bidhaa ili waendelee kuzalisha na kuuza.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga ameitaka Halmashauri ya Mji wa Masasi kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati, akisisitiza kuwa kuongeza muda wa miradi mara kwa mara hakusaidii kuongeza tija, amesema wakandarasi wanapaswa kuongeza nguvu kazi na kasi ya utekelezaji.

Akizindua kiwanda darasa cha kubangua korosho cha CAMARTEC katika Kijiji cha Mandiwa, Masasi, chenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600, Kapinga amesema Serikali inaendelea kuimarisha mnyororo wa thamani wa korosho ili kuongeza kipato cha wakulima na kufungua fursa za ajira.

Msimamizi wa kiwanda hicho, Mhandisi January Mlomo, amesema kina uwezo wa kubangua tani 3.15 za korosho kwa siku na tani 700 kwa mwaka, huku zaidi ya wanafunzi 1,000 wakitarajiwa kupata mafunzo ya ubanguaji kila mwaka. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amewataka wananchi kutumia fursa hizo na kuwekeza kwenye suala la kuhakikisha watoto wanapata elimu.

Waziri Kapinga yupo Mtwara kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo anazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo serikali inalenga kuongeza nafasi ya sekta binafsi katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button