SERIKALI imeongeza kasi katika vita dhidi ya mifuko ya plastiki na imekamata tani 41 za mifuko hiyo katika kiwanda kinachomilikiwa na raia wa China ambacho kimetozwa takribani Sh milioni 100 kama faini.
Oparesheni hiyo inatekelezwa na mamlaka mbalimbali kupitia wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na kamati za ulinzi na usalama katika masoko, minada, maduka ya samaki na ya nyama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo alisema Alhamis kuwa, kuanzia sasa yeyote atakayekamatwa na mifuko hiyo atatozwa faini na gharama za uteketezaji wa mifuko hiyo.
“Juzi tumekamata kiwanda cha Wachina kikizalisha mifuko pamoja na shehena tuliyoidhibiti na kumtoza faini ikiwemo gharama za kuiteketeza mifuko hiyo, pia tumempa muda wa wiki moja kuwasiliana na aliowauzia wairejeshe mifuko yote na aiteketeze kwa gharama zake,” alisema Dk Jafo.
Alisema pia alitoa maelekezo kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo walionunua mifuko hiyo wairejeshe walikonunulia ndani ya wiki moja kuanzia juzi.
Alisema tani 41 za mifuko walizozikamata ziliteketezwa jana katika Kiwanda cha Saruji Wazo ambako ndiko kuna mashine zinazofaa kuteketeza mifuko hiyo.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Dk Jafo alisema tangu serikali izuie matumizi ya mifuko ya plastiki, kumekuwa na mafanikio lakini sasa tatizo limeanza kurudi.
Alisema hayo wakati wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) walipokutana kujadili utekelezaji wa sheria ya mazingira.
Dk Jafo aliagiza ifanyike oparesheni kuhakikisha mifuko ya plastiki haionekani tena mitaani na oparesheni hiyo iguse masoko, magulio, madukani na bucha za samaki na nyama.
Katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, mifuko hiyo imeanza kutumika kwa wingi kwenye masoko, mabucha na hata mitaani mkoani Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alitoa agizo la kuanza msako wa kukamata mifuko ya plastiki katika masoko mkoani humo akiwaagiza viongozi wa masoko kutekeleza agizo hilo.
Makalla alisema mifuko hiyo inazalishwa kiholela hivyo hailipiwi kodi na walioruhusiwa kuizalisha mifuko mbadala wanafunga viwanda kutokana na kuwepo utitiri wa mifuko ya plastiki.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka alikiri vifungashio vya plastiki kurudi kwa nguvu pamoja na jitihada kubwa wanazozifanya za kuvidhibiti kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
“Kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna nchi hazijaweka zuio la mifuko ya plastiki hivyo inaingia nchini kupitia mipakani. Kwa hiyo tunapata changamoto nyingi Kanda ya Ziwa, mikoa ya Kaskazini, Kusini na Magharibi. Tatizo limezidi kuwa kubwa kwa kuwa vifungashio hivi vinavyoingia sokoni tunapambana na mifuko rahisi kwa gharama ndogo,” alisema Dk Gwamaka.
Juni Mosi, mwaka 2019, serikali ilianza utekelezaji wa katazo kuhusu uzalishaji, uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.
Katazo hilo linatokana na athari ya mifuko hiyo katika mazingira kwa kuwa inakadiriwa hukaa hadi zaidi ya miaka 500 bila kuoza.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na kanuni zake za mwaka 2019 inabainisha uzalishaji na uagizaji adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni tano na isiyozidi Sh milioni 20, kifungo kisichozidi miaka miwili jela au adhabu zote mbili kwa pamoja.
Pia, kwa mujibu wa sheria hiyo, kuhifadhi na kusambaza mifuko adhabu zake ni faini isiyopungua Sh milioni tano na isiyozidi Sh milioni 52, kifungo kisichozidi miaka miwili au faini na kifungo kwa pamoja.
Ukipatikana na hatia ya kuuza mifuko ya plastiki adhabu ni faini isiyopungua Sh 100,000 na isiyozidi Sh 500,000, kifungo kisichozidi miezi mitatu jela au adhabu zote mbili kifungo na faini.
Na mtu anayetumia mifuko hiyo ya plastiki adhabu yake ni faini isiyopungua Sh 30,000 na isiyozidi Sh 200,000, kifungo kisichozidi siku saba au faini na kifungo.