Mahindi kilo 335,238 yauzwa mnada wa kwanza kidijitali

RUKWA: Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), imeendesha mnada wa kwanza wa mahindi meupe Tanzania kwa kutumia mfumo wa mnada wa kidijitali, hatua inayolenga kuimarisha uwazi na ushindani katika biashara ya zao hilo.

Katika awamu ya kwanza ya mnada huo uliofanyika mkoani Rukwa, jumla ya kilo 335,238 za mahindi meupe zimeuzwa kupitia mfumo huo wa kidijitali.

Kabla ya kuwasilishwa kwenye mnada, mahindi hayo yalifanyiwa ukaguzi na upimaji wa ubora na kiasi na SGS, kampuni ya kimataifa inayojihusisha na ukaguzi, upimaji na uthibitishaji.

Vipimo vilijumuisha kiwango cha unyevu na sumukuvu (aflatoxin), hatua iliyosaidia kuweka taarifa sahihi kuhusu ubora wa mahindi na kuwawezesha wanunuzi kufanya tathmini kabla ya kuwasilisha zabuni zao.

COPRA imesema matumizi ya mifumo rasmi ya biashara ya mazao ni sehemu ya juhudi za kuongeza uwazi katika bei na taarifa za masoko, kudhibiti ubora katika hatua ya ununuzi na kuimarisha uhusiano kati ya wazalishaji, wauzaji na wanunuzi.

Aidha, mamlaka hiyo imeeleza kuwa kuimarisha ubora na viwango vya mazao ni muhimu katika kuongeza upatikanaji na kulinda masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Mnada huo uliandaliwa na COPRA kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) na Bodi ya Stakabadhi za Ghala Tanzania (WRRB), huku ukiungwa mkono na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

COPRA imeeleza kuwa awamu nyingine za minada ya zao la mahindi zitaendelea kutangazwa kadri zitakavyoandaliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button