Makubaliano TPSF, DSE kuimarisha ushindani biashara

DAR ES SALAAM: Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limesaini rasmi Hati ya Makubaliano (MoU) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha ukuaji na ushindani wa biashara za Tanzania kupitia kujengea uwezo wafanyabiashara na kuongeza fursa za upatikanaji wa mitaji na uwekezaji.

Ushirikiano huu unaweka mfumo wa pamoja wa kutekeleza Programu ya DSE Enterprise Acceleration Program (DEAP) pamoja na jukwaa la ENDELEZA. Kupitia programu hizi, wanachama wa TPSF watanufaika na mafunzo ya maendeleo ya biashara, ushauri elekezi (mentorship), utambuzi wa biashara zao, pamoja na kuunganishwa na wawekezaji na taasisi za kifedha.

MoU hii pia inalenga kuziwezesha biashara kuwa tayari kwa uwekezaji kwa kuwajengea uwezo katika maeneo muhimu kama uandaaji wa mipango ya biashara inayovutia wawekezaji, utawala bora wa kampuni, tathmini ya biashara, mbinu za kupata mitaji, pamoja na stadi nyingine muhimu za kukuza biashara.

Kupitia ushirikiano huu, TPSF na DSE zitashirikiana kuhamasisha ushiriki wa wafanyabiashara nchini kote, kukuza programu hizi, na kuimarisha mazingira ya ujasiriamali nchini kwa kuwezesha SMEs kukua, kuvutia uwekezaji, na kuchangia maendeleo endelevu ya uchumi wa Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button