Mambo yaiva kampeni kusogeza huduma za gesi

DAR ES SALAAM: Kampuni ya Puma Energy Tanzania imezindua rasmi ziara ya PumaGas itakayopita katika mikoa mitano nchini kwa kipindi cha wiki nane, ikiwa na lengo la kusogeza huduma za gesi ya kupikia karibu na kaya na wafanyabiashara.

Ziara hiyo imezinduliwa katika kituo kipya cha Puma Energy kilichopo Bunju, Dar es Salaam, na itapita katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma kabla ya kuhitimishwa jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, ziara hiyo inalenga kuwafikia watumiaji wa gesi ya kupikia katika maeneo mbalimbali na kuwapa fursa ya kupata taarifa kuhusu matumizi ya gesi, bidhaa na huduma zinazotolewa na PumaGas, pamoja na kuwasiliana moja kwa moja na mawakala wa kampuni katika maeneo yao.

Ziara hiyo imebeba ujumbe wa kampeni ya “Hakuna Kuchochea, Tumerahisisha na PumaGas,” unaolenga kuhamasisha matumizi ya gesi ya kupikia katika shughuli za kila siku za kaya na biashara.

Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Puma Energy Tanzania, Lilian Kanora, alisema kampuni hiyo inalenga zaidi ya kutoa elimu kuhusu gesi kwa kuwawezesha wananchi kuifahamu na kuona namna inavyoweza kutumika katika shughuli zao za kila siku.

“Lengo letu si kuwaambia watu kuhusu gesi ya kupikia pekee, bali kuwapa nafasi ya kuifahamu, kuona namna inavyotumika na kupata taarifa wanazohitaji kabla ya kufanya uamuzi,” alisema Kanora.

Alisema kwa kupeleka PumaGas moja kwa moja kwenye jamii, kampuni inalenga kuwa karibu zaidi na wateja na kuelewa mahitaji yao katika maeneo mbalimbali.

Katika vituo vitakavyofikiwa na ziara hiyo, timu za PumaGas zitakutana na kaya, wafanyabiashara wa chakula, migahawa, hoteli na mawakala wa gesi.

Pia kutakuwa na maonesho ya matumizi ya gesi pamoja na fursa kwa wananchi kuuliza maswali kuhusu matumizi, upatikanaji na ujazaji wa gesi kwenye mitungi.

Kwa wafanyabiashara wanaotumia gesi katika shughuli zao, ziara hiyo itatoa elimu kuhusu matumizi ya gesi katika biashara mbalimbali, ikiwemo kwa mama ntilie, wauza chipsi, migahawa na hoteli.

Mawakala wa gesi nao watashirikishwa katika juhudi za kuimarisha upatikanaji wa bidhaa na huduma za PumaGas kwa wateja katika maeneo yao.

Hatua muhimu ya ziara hiyo itakuwa jijini Mwanza, ambako Puma Energy inatarajia kuingia rasmi katika soko la Kanda ya Ziwa.

Uzinduzi huo utahusisha hafla ya kutambulisha PumaGas katika soko hilo, kukabidhi mtungi kwa mteja wa kwanza na kumtambua wakala wa kwanza wa PumaGas katika eneo hilo.

Aidha, uzinduzi huo utahusisha wadau na vyombo vya habari pamoja na maonesho ya matumizi ya gesi katika shughuli za kawaida za kila siku.

Katika maonesho hayo, mama ntilie atapika chapati kwa kutumia mtungi wa PumaGas, huku wananchi wakipata fursa ya kuona kwa vitendo kiasi cha chakula kinachoweza kuandaliwa kwa kutumia gesi hiyo.

Puma Energy imesema ziara hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kuongeza upatikanaji wa gesi ya kupikia na kuifikisha huduma hiyo kwa wananchi katika maeneo mengi zaidi nchini.

Kwa kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza, kampuni hiyo inatarajia kutumia ziara hiyo kukutana na jamii mbalimbali, kusikiliza mahitaji ya watumiaji na kusogeza huduma za PumaGas karibu na maeneo wanayoishi na kufanya biashara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button