Maridhiano, amani ni msingi wa maendeleo

MCHAMBUZI wa masuala ya siasa, maridhiano na amani ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya AFREDA ya Kijamii na Uchumi, Denisi Mchunguzi amesema maridhiano na amani ni nguzo muhimu za kujenga umoja na maendeleo ya taifa hivyo vinapaswa kulindwa na kuendelezwa kwa ushiriki wa makundi yote ya jamii.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Dailynews Digital jijini Dar-es-salaam, Mchunguzi amesema mchakato wa maridhiano haupaswi kuwa wa viongozi pekee bali uwahusishe wananchi wote bila kujali tofauti zao za kisiasa, kijamii au kiuchumi. SOMA: Serikali yaja mpango wa kitaifa wa maridhiano
Amesema makundi yanayopaswa kushirikishwa ni pamoja na wanawake, vijana, watu wenye ulemavu, watoto, wanafunzi na viongozi wa jadi ili kuhakikisha kila kundi linatoa mchango wake katika kuimarisha umoja wa kitaifa. “Maridhiano yanajenga kuaminiana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuweka mazingira bora ya maendeleo. Ni muhimu kila Mtanzania akashiriki katika mchakato huo kwa nafasi yake,” amesema.
Hatahivyo, ameonezea kuwa Katiba ya Tanzania imeweka msingi wa kulinda amani ambayo imeendelea kuwa moja ya tunu muhimu za taifa na kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. “Amani ndiyo inayowawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kila siku kwa uhuru na usalama. Ni wajibu wa kila Mtanzania kuendelea kuilinda na kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.
Aidha amewataka wananchi kujiepusha na kauli au vitendo vinavyoweza kuchochea migawanyiko na badala yake kuendeleza mazungumzo, kuvumiliana na kushirikiana katika kujenga taifa lenye umoja na maendeleo.Amesema tofauti za kimtazamo ni jambo la kawaida katika jamii, lakini zinapaswa kushughulikiwa kwa njia za mazungumzo na kuheshimiana ili kuendelea kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa.



