Serikali yaendelea kusisitiza tahadhari ya El Nino

DODOMA: WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo, amezitaka mamlaka za miji, taasisi na wananchi kuchukua hatua za maandalizi kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
Dk Akwilapo alitoa rai hiyo jjijini Dodoma wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika chini ya kaulimbiu ya “Makazi Toshelezi kwa Wote.”

Alisema uzoefu wa mafuriko yaliyowahi kutokea nchini ni ukumbusho wa umuhimu wa kuchukua hatua mapema ili kulinda maisha ya wananchi, makazi na miundombinu.
“Tusisubiri mvua inyeshe ndipo tuanze kuchukua hatua, kila mmoja wetu aanze sasa. Mamlaka za miji na taasisi zote zizingatie hatua zote zilizoelekezwa na mamlaka za nchi ili kupunguza athari za janga hili.”
Akizungumzia makazi bora, Dk Akwilapo alisema makazi toshelezi si kuwa na nyumba pekee, bali yanahusisha nyumba salama, ardhi iliyopangwa, huduma muhimu, usalama wa miliki, miundombinu imara na mazingira yanayoweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi.

Alisema ongezeko la watu na kasi ya upanuzi wa miji linahitaji mipango madhubuti ya kuhakikisha maeneo ya makazi yanapangwa na kuendelezwa kwa kuzingatia usalama wa wananchi na uwezo wa kukabiliana na changamoto, ikiwemo mafuriko.
Alisema Serikali inaendelea kuboresha Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 ili iendane na mahitaji na changamoto za sasa.
Kwa mujibu wa Dk Akwilapo, hatua hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ajenda Mpya ya Miji na Lengo la 11 la Maendeleo Endelevu (SDG 11).

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi, Deogratias Kalimenze alisema siku hiyo ni fursa ya kutafakari hali ya makazi nchini na hatua za kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, salama na yenye gharama nafuu.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN-Habitat), Dk Grace Lubaale, alisema ukuaji wa miji unaongeza mahitaji ya nyumba, ardhi iliyopangwa, miundombinu na huduma za msingi, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau.



