WAAGIZAJI , wasambazaji na mawakala waliosajiliwa kufanya biashara ya kupeleka mbegu maalum za ruzuku mkoani Manyara wameagizwa kufuata miongozo ya serikali katika kuuza mbegu bora ya mahindi kwa ruzuku
Pia wamehimizwa kuuza mbegu bora ya mahindi ya ruzuku kwa bei elekezi ya Sh 14,000 kwa mfuko wa kilo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Babati mkoani Manyara, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amebainisha kuwa bei elekezi imewekwa kwa mujibu wa miongozo ya uuzaji na kwamba atakayekiuka mkoa umejipanga kufanya ukaguzi wa zoezi hilo.
Amesema serikali kupitia maboresho ya sekta ya kilimo yataongeza kipato cha mkulima, kuimarisha usalama wa chakula, upatikanaji wa pembejeo na mbegu bora za mahindi za ruzuku katika ngazi ya kaya.
“Mageuzi yanapomnufaisha mkulima pia yananufaisha taifa kwa kupata uhakika wa usalama wa chakula cha kutumia na kupata ziada ya kuuza,”amebainisha Sendiga.
“Ongezeko la bajeti la mwaka huu wa fedha la Sh trilioni 1 ni Sehemu ya mageuzi ya kilimo inaboresha ruzuku za mbolea,mbegu na vitendea kazi ”
Kwa mujibu wake mbegu bora za mahindi zinazokwenda kuuzwa kwa ruzuku ni mbegu bora zilizothibitishwa tayari kutekelezwa katika msimu wa mwaka 2024/2025.
Aidha amefafanua kuwa mbegu zinazochavushwa zitauzwa kwa Sh 7,000 kwa mfuko wa kilo mbili.
Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia sehemu za uchumi na uzalishaji, Faraja Ngerageza amesema kupitia mpango huo wa ruzuku ya mbegu bora ya mahindi zaidi ya wakulima 30,000 watanufaika mkoani humo.