Mbunge awashika mkono waathirika mvua za upepo

MBUNGE wa Jimbo la Buhigwe lililopo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Felix Kavejuru amewashika mkono wananchi wa kijiji cha Kigogwe wilayani humo walioathiriwa na mvua za upepo baada ya paa za nyumba zao kuezuliwa na upepo na nyingine kuanguka.
Kavejuru alifika kijijini hapo kuwapa mkono wa pole wananchi hao mwishoni mwa wiki iliyopita na kueleza kuwa ameguswa na kadhia iliyowapa hivyo kusaidia kidogo alichonacho ili kuwapa faraja wahanga hao.


Baadhi ya nyumba zilizoathiriwa na mvua katika kijiji cha Kigogwe Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma
Akiwa kijijini hapo mbunge huyo alitoa Sh 50,000 kwa kila kaya iliyoathiriwa na mvua hiyo akiahidi pia kutoa bati kwa ofisi ya CCM tawi la Kigogwe na kanisa la Sabato ambayo yaliezuliwa paa zake.
Akitoa taarifa ya maafa hayo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kigogwe wilayani Buhigwe, Methusela Ntahonsigaye amesema kuwa jumla ya watu 25 wameathiriwa na mvua hiyo kwa nyumba zao kuezuliwa paa, nyingine kuanguka lakini pia watu watatu wajeruhiwa ambapo tayari Mkuu wa Wilaya Buhigwe, Michael Ngayalina ameshatembelea eneo hilo kuona madhara yaliyotokea ili kuona hatua za kuchukua.

Mbunge wa jimbo la Buhigwe Felix Kavejuru (kushoto) akitoa mkono wa pole kwa wananchi wa kijiji cha Kigogwe wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Felix Mathias (m ambao nyumba zao zilipata madhara ya mvua ya upepo wiki iliyopita.
Mmoja wa waathirika wa mvua hiyo, Stephano Ezekiel amesema kuwa wakati mvua inanyesha alikuwa ndani na familia ghafla akaona upepo na mvua kubwa inanyesha ambapo ukutwa ulianguka hivyo kulazimika kukimbia kwa majirani kuomba hifadhi.



