Mbunguli maji hayatoki bili zinatoka
DAR ES SALAAM: WANANCHI wa Mtaa wa Mbunguli, kata ya Saranga iliyopo Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam wameandamana wakilalamikia ukosefu wa huduma ya maji kwa zaidi ya mwaka mmoja huku wakiendelea kutumiwa bili za maji.
Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari hii leo katika ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) eneo la Tabata Kinyerezi, wananchi hao wamesema tatizo la maji limeanza Mei mwaka jana na hakuna ufumbuzi huku wasoma mita wakiendelea kutembelea na kutuma bili hewa.
Mjumbe wa Shina Namba 3 katika mtaa huo, Fadhila Kikwesha amesema ukosefu wa maji umesababisha maisha kuwa magumu, huku baadhi ya wananchi wakimlaumu yeye kuhusika na tatizo hilo, hali iliyoleta mgogoro wa kijamii.
Mkazi wa eneo hilo, Tutindaga Mwaisunga amesema tatizo hilo linawesababishwa na baadhi ya wafanyakazi wa DAWASA ambao hawatimizi majukumu yao ipasavyo. Aliongeza kuwa kuna watu wanaotumia fursa hiyo kuuza maji kwa bei ya juu, hali inayoongeza mateso kwa wananchi wa kawaida.
SOMA: DAWASA yaanza kutekeleza agizo la Rais Samia
Mkazi mwingine, Asia Said ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo, wakazi wengi wanalazimika kutumia maji yasiyo salama kutoka mitaroni kwa shughuli za kila siku kama kuoga, hali inayosababisha kuongezeka kwa magonjwa kama UTI na vipele.
Tilbart Litego ameeleza kuwa ukosefu wa maji umeathiri familia nyingi, huku wanawake wakilazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji, jambo ambalo limeleta changamoto katika majukumu mengine ya kifamilia.
Supora Jackson alionya kuwa hali ya wasoma mita kuendelea kupita kwenye mtaa huo na kutuma bili bila maji ni kero kubwa, na inaweza kusababisha vurugu iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Everlasting Lyaro, alitoa wito kwa wananchi kuwa na subira, akibainisha kuwa mhandisi anayehusika atatembelea eneo hilo hivi karibuni ili kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa ifikapo Ijumaa.
SOMA: DAWASA yaanza kusafisha visima Dar
Aliahidi kuwa huduma ya maji itarejea kwa kaya zote zilizounganishwa na mabomba.
Kamati ya Kudumu Bunge Maji na Mazingira imetembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa Usafi wa Mazingira katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na kuridhika na kasi ya utekelezaji… pic.twitter.com/XumFkdCCQY
— DAWASA (@dawasatz) September 14, 2024