DAWASA yaanza kutekeleza agizo la Rais Samia

DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maji Jumaa Aweso kuwarudishia huduma ya maji wateja waliositishiwa huduma kwa msamaha wa kutolipa pesa ya faini ya kurudishiwa huduma alilolitoa mapema wiki hii kwenye vyombo vya habari.

Aweso akitoa agizo hilo alisema lilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassani katika salamu za kilele cha Wiki ya Maji kwa kuagiza kuondoa faini na msamaha kwa kipindi cha mwezi mmoja, huku mteja akiwajibika kulipa sehemu ya deni lake tu.

Akizungumza wakati wa utekelezaji wa agizo katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, Maria Sanga mkazi wa Kijiji cha Wavuvi, Kata ya Kurasini amesema: “Nyumbani kwangu tulisitishiwa huduma ya maji kwa miaka mingi sababu ya deni kubwa tukashindwa kulipa bili, tumeteseka muda mrefu bila ya maji ya uhakika lakini tunamshukuru sana Rais Samia kupitia Waziri wa Maji, kwa kutoa msamaha wa faini ya kurudishiwa maji bila ya faini pamoja na kuturuhusu kulipa deni kidogo kidogo huku tukiendelea kufurahia huduma ya maji.”

Kwa upande wake , Sarah Herman mkazi wa Kata ya Yombo amesema: “Maisha ya sasa ni magumu, tulisitishiwa huduma ya maji sababu ya kulimbikiza malipo ya bili za maji, lakini jana tulipunguza deni na leo tumeona DAWASA wamekuja kurudisha maji bure bila ya kulipa faini, hii imetusaidia kuokoa pesa na kusaidia kufanya matumizi mengine ya kujikimu na maisha.”

Msamaha huu wa kutolipa faini ya kurudishiwa huduma ya maji itakuwepo kwa muda wa siku 30 kuanzia mwezi Machi hadi Aprili, 2024 kwa mamlaka za maji nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button