KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), wameanzisha oparesheni maalumu ya kuondoa zaidi ya mifugo 200,000 iliyovamia eneo la ardhi oevu ya Bonde la Ihefu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wilayani Mbarali.
Mifugo hiyo iliyoingizwa na wafugaji kinyemela kwenye eneo hilo, inahatarisha ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na Mto Ruaha Mkuu.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alisema hayo Mbarali baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa kushirikiana na maofisa wa hifadhi hiyo kutembelea eneo hilo kukagua uharibifu wa mazingira unaoendelea.
Viongozi hao walikagua eneo hilo kwa kutumia ndege na kushuhudia makundi makubwa ya mifugo yakiwa yamechanganyika na wanyamapori kama tembo na pofu.
Aidha, walikuta mifugo zaidi ya 500 imekamatwa na askari wa Jeshi USU ikiwa imehifadhiwa kwenye Kambi ya Ikoga Mpya ikidaiwa ilisagwa umbali wa zaidi ya kilometa 20 ndani ya hifadhi.
Homera alisema hali hiyo inahatarisha uwepo wa hifadhi hiyo ambayo ni miongoni mwa hifadhi kubwa pamoja na Mto Ruaha Mkuu ambao ni muhimu kwa maisha ya viumbe hai pamoja na miradi mikubwa ya umeme ukiwamo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere, Rufiji.
Kutokana na hali hiyo, aliagiza ndani ya siku 10 mifugo yote iwe imeondolewa hifadhini kwa ushirikiano kati ya maofisa wa hifadhi na kikosi kazi kitakachoundwa na vyombo vya dola.
Alisema mbali na kuiondoa mifugo hiyo, pia uchunguzi utafanyika ili kuwabaini viongozi wanaoruhusu mifugo hiyo kuingizwa kwenye eneo hilo na kwamba kuna viashiria vya baadhi ya viongozi kupokea rushwa.
“Hii hali haikubaliki, sasa hii mifugo yote lazima iondolewe ndani ya siku kumi na leo (juzi) ndio tunazindua zoezi lenyewe, hapa kwetu kuna vitalu vya Narco lazima tufanye uchunguzi ili kujua ni akina nani wanaomiliki vitalu hivyo ili ikiwezekana wafugaji wapelekwe huko,” alisema Homera.
Aliiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na viongozi wa mkoa kuboresha hali ya ufugaji ili kupunguza migogoro iliyopo, akiahidi kuwasiliana na waziri mwenye dhamana hiyo, Mashimba Ndaki.
Akitoa taarifa ya uvamizi wa bonde hilo la Ihefu, Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Ole Meng’ataki alisema katika kipindi cha miaka miwili wamekamata mifugo 12,758 ambayo ilikuwa inaingizwa ndani ya hifadhi hiyo.
Alisema baada ya kukamata mifugo hiyo wamekuwa wakiwatoza faini wafugaji hao na katika kipindi hicho wamekusanya zaidi ya Sh bilioni 1.2 na licha ya kulipa faini, wafugaji hao wamekuwa wanarejesha mifugo hiyo.
Alisema mifugo hiyo ilikamatwa katika matukio 53 na yote katika Bonde la Ihefu ambalo ni chanzo kikuu cha Mto Ruaha Mkuu na licha ya kukabiliana na wafugaji hao, wamekuwa wakitumia silaha za jadi kujihami.
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune alisema eneo ililotengwa kuchungia katika wilaya hiyo ni hekta 12 ambazo zinatosheleza mifugo isiyozidi 60,000, lakini wilaya hiyo ina mifugo zaidi ya 200,000.