Mikakati kuboresha stakabadhi ghalani imekuja wakati mwafaka

WIZARA ya Viwanda na Biashara imekuja na mikakati minne yenye lengo la kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa msimu wa mwaka 2025/2026.

Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, katika kuimarisha mfumo huo, wizara kupitia Bodi ya Stakabadhi za Ghala (WRRB), imepanga kuendelea kuboresha mfumo huo kwa kupanua utekelezaji wake
katika maeneo mapya ili kuongeza tija kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo.

Dk Jafo amesema kuwa kupitia bodi, juhudi za kuhamasisha matumizi ya mfumo huo zitaimarishwa sambamba na
kutatua changamoto na kero zilizojitokeza msimu uliopita.

Advertisement

Mikakati mingine kwa mujibu wake ni bodi kukamilisha kwa haraka mchakato wa kupata ithibati ya Benki Kuu
kuhusu mwongozo utakaosimamia utendaji wao ili uanze kutumika kwa lengo la kuondoa changamoto ya hasara ambazo baadhi ya taasisi za fedha zimekuwa zikikutana nazo.

Ameitaja pia kupanua matumizi ya Meneja Dhamana hususani katika biashara ya nafaka ili kuchochea usindikaji wa mazao, kuongeza thamani na kuimarisha ajira katika maeneo ya vijijini, na kuendeleza urasimishaji wa bidhaa mpya na ambazo hazijatumia kikamilifu mfumo ikiwamo zao la kahawa.

Amehimiza na kuwakaribisha wadau hususani sekta binafsi, halmashauri za miji, manispaa na majiji kuwekeza
katika ujenzi wa ghala za kisasa katika maeneo yanayotekeleza mfumo wa stakabadhi za ghala.

Mikakati hii iliyotajwa na wizara ni muhimu na imekuja katika wakati mwafaka kutokana na ukweli kwamba stakabadhi ya mazao ghalani imefanya vizuri katika maeneo na mazao ambayo yalianza kutumia mfumo huu.

Moja ya mafanikio ya mfumo ni mauzo ya mazao hayo kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala yamesaidia upatikanaji wa bei nzuri ya soko kutokana na ushindani wa wanunuzi na hivyo kuwanufaisha wakulima wa maeneo
husika.

Kwa mfano, bei ya kakao kabla ya mfumo ilikuwa Sh 2,500 na baada ya mfumo bei ilikuwa Sh 32,000 kwa kilogramu; ufuta bei kabla ya mfumo ilikuwa Sh 500 hadi Sh 800 baada ya mfumo bei iliongezeka na kuwa Sh 2,800 hadi Sh 4,500 kwa kilogramu.

Kama ilivyo kazi ya WRRB ya kusimamia na kuhamasisha matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani unaohakikisha usawa na uendelevu wa upatikanaji wa mikopo na mifumo ya masoko, tunafarijika kuona serikali inazidi kuweka mikakati ya kuimarisha mfumo na kutanua wigo kwa kurasimisha bidhaa mpya.

Ni imani yetu kwamba Bodi ya Stakabadhi ya Ghala itasimamia kikamilifu utekelezaji wa mikakati hii ili kuja na
matokeo chanya na kusaidia wakulima na taifa kwa ujumla katika masuala ya masoko na uuzaji wa mazao, na hivyo
kuchangia kukuza uchumi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *