Mil 200/- zakarabati mabweni shule Ilboru

KUTOKANA na mpango mkakati wa serikali wa kuboresha miundombinu ya elimu hususani kwenye shule kongwe nchini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa EP4R imetoa Sh milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa mabweni Shule ya Sekondari Ilboru, Halmashauri ya Arusha.

Akizungumza wakati wa kukagua maendeleo ya mradi huo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, alisema kiasi hicho cha fedha kutoka serikali kuu kimewezesha ukarabati wa mabweni manne ya Ilboru na tayari utekelezaji wa mradi huo upo hatua za mwisho za ukamilishaji.

Alishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo kwa kuwa mabweni ya shule hiyo yalikuwa kwenye hali ya uchakavu  uliotokana na kujengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.

“Tumeanza mwaka mpya wa fed

ha 2022/2023 vizuri, mwishoni Julai tumepokea fedha hizo za ukarabati wa mabweni ya shule yetu kongwe ya Ilboru, ukarabati huu utawezesha wanafunzi kulala kwenye mazingira rafiki,” alisema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Ilboru, Denis Otieno, alisema fedha hizo zimekuja wakati mwafaka kwa kuwa mabweni hayo yalikuwa yamechakaa. Alisisitiza kuwa ukarabati huo ni wa msingi kwa wanafunzi na shule kwa ujumla wake.

“Mabweni yalikuwa yamechoka, yalijengwa mwaka 1963, ukarabati huu utasaidia watoto kulala kwenye mazingira safi na rafiki, jambo ambalo tunaamini litakuwa na matokeo makubwa kitaaluma katika shule yetu,” alisema.

Alifafanua kuwa Sh milioni 200 zinatumika kukarabati mabweni manne, ikiwamo kubadilisha mapaa, kubadilisha mifumo ya maji safi na maji taka, mfumo wa umeme, kubadilisha milango, madirisha na vioo vya madirisha, kukarabati vyoo, kuziba nyufa pamoja na kupaka rangi ndani na nje ya majengo hayo.

“Tunaishukuru serikali kwa kuwa mabweni yote manne yanalaza jumla ya wanafunzi 760, huku kila bweni likilaza wanafunzi 190, kwa mazingira bora ya kulala ni uhakika wa afya za wanafunzi na taaluma,” alisema.

Shule ya Sekondari Ilboru ni shule ya wavulana na ni miongoni mwa shule kongwe nchini yenye wanafunzi 860, inayofanya vizuri kitaaluma kwa kushika nafasi 10 bora kitaifa kwa matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha nne na cha sita.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button