Mil 356/- kupeleka maji kwa wananchi 2,427 Simiyu

HALMASHAURI ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu imetumia shilingi milioni 356 katika ujenzi wa mradi wa maji safi na salama utakaonufaisha wakazi takribani 2,427 wa Kijiji cha Isengwa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda alisema upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo hayo utapunguza adha kwa wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata maji kwenye mito.

Alisema upatikanaji maji safi na salama kwa wakazi wa Mkoa wa Simiyu ni kipaumbele katika serikali na lengo ni kuhakikisha wanafikia asilimia 85 ya wakazi wa mijini na asilimia 75 kwa wakazi wa vijijini katika mkoa huo.

Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26, umeweka kipaumbele katika upatikanaji na usambazaji wa majisafi na salama vijijini na mijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeielekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa mijini inakuwa asilimia 95 na vijijini inakuwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Meatu, George Masawe alisema mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 25,000 za maji kwa siku.

“Mahitaji ya maji Isengwa ni lita 20,675 kwa siku huku uzalishaji wa chanzo ukiwa lita za ujazo 1,025,000 kwa siku na hivyo kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi wote wanaoishi katika kijiji hicho na kuongeza upatikanaji wa maji wilayani hapo kwa asilimia 0.8 na hivyo kufikia asilimia 68.1,” alisema Masawe.

Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Simiyu, Mariam Majala alisema ni muhimu chombo cha watumiaji wa maji ngazi ya jamii kikazingatia bei elekezi zilizotangazwa.

Majala alisema bei ya maji kwa wanaotumia nishati ya jua ndoo ni Sh 30, jenereta ndoo ni Sh 50 na umeme ndoo Sh 40.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button