Miradi ya bil 277/- kuwatua ndoo Kanda ya Ziwa

Miradi ya bil 277/- kuwatua ndoo Kanda ya Ziwa

JUMLA ya Euro milioni 104.5 sawa na Sh bilioni 276.925 zimetumika katika miradi ya majisafi na usafi wa mazingira katika Jiji la Mwanza na miji ya Bukoba, Musoma, Misungwi, Lamadi na Magu mkoani Mwanza.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (Mwauwasa), Leonard Msenyele alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo alipozungumza na HabariLEO.

Msenyele alisema miradi hiyo inatekelezwa kupitia Programu ya Uboreshaji wa Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira (LVWATSAN) iliyolenga kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwenye miji hiyo.

Advertisement

Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26, umeweka kipaumbele katika upatikanaji na usambazaji wa majisafi na salama vijijini na mijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

Mpango huo umelenga kuhakikisha asilimia 95 ya idadi ya watu katika Jiji la Dar es Salaam na makao makuu ya mikoa wanapata maji ya bomba au maji yanayolindwa kama chanzo kikuu.

Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeelekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa mijini inakuwa asilimia 95 na mijini inakuwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Msenyele alisema programu hiyo inatekelezwa na serikali ya Tanzania na washirika wa maendeleo Benki ya Uwekezaji Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.

Alisema huduma za maji katika Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela na miji ya Misungwi, Magu, Ngudu na Nansio inatolewa na Mwauwasa kwa kutumia vyanzo vya maji vilivyopo mwambao wa Ziwa Victoria katika maeneo ya Capri Point (Mwanza), Nyahiti (Misungwi), Busulwa (Magu), Ihelele na Nebuye Nansio.

Msenyele alisema mitambo ya uzalishaji wa maji iliyopo katika eneo la Capri Point ina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 106 sawa na lita 108,000,000 kwa siku na kwa sasa mamlaka inazalisha wastani wa  mita za ujazo 90,000 sawa na lita milioni 90 kwa siku.

“Mamlaka ina mtandao wa mabomba ya maji wenye urefu wa kilomita 1,200 unaohudumia asilimia 90 ya maeneo ya jijini Mwanza,” alisema na kuongeza kuwa kwa maeneo ya mjini na pembezoni huduma hiyo inawafikia wakazi kwa asilimia 75,” alisema.

Msenyele alisema yamejengwa matangi ya kuhifadhia maji yenye jumla ya mita za ujazo 33,400 ikihudumia jumla ya wateja 93,490 waliofungiwa dira za maji.

“Mamlaka ina jumla ya magati 438 ya maji yaliyojengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye kipato kidogo,” alisema.

Msenyele alisema mamlaka pia inatoa huduma za uondoshaji wa majitaka kwa jumla ya kaya 5,000 zilizounganishwa kwa kutumia mtandao wa mabomba yenye urefu wa kilomita 133 pamoja na mabwawa 13 ya kutibu majitaka yaliyoko eneo la Butuja katika manispaa ya Ilemela.

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *