Miradi ya bil 5.6/- kuboresha elimu Mwanza

HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza kuanzia Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu imetekeleza miradi ya elimu yenye thamani ya Sh bilioni 5.6 kuboresha elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sekiete Yahaya alisema hayo alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa huduma za jamii na miradi ya elimu ya msingi na sekondari.

Yahaya alisema katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa upande wa sekta ya elimu ya msingi,  kuanzia Juni mwaka jana hadi Juni mwaka huu, halmashauri hiyo ilipokea Sh 353,124,000 kutoka serikali kuu, wahisani na michango ya wananchi kutekeleza miradi kwenye sekta ya elimu msingi.

Katika Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020  kipengele cha elimu, imezungumzia  chama kitakavyosimamia kustawisha maisha ya kila Mtanzania, kutokomeza umasikini na kuhakikisha taifa linafikia uchumi wa kati.

Vipaumbele vikuu vya serikali za CCM katika miaka mitano kuanzia 2020 hadi 2025 ni kuimarisha elimu, kuboresha  mfumo wa elimu ili uweze kuzalisha wataalamu mahiri zaidi wenye uwezo, wakaotaweza kujiajiri na kuajirika popote.

Ilani imeeleza kuwa itaimarisha ubora wa elimu kwa kuhakikisha kunakuwapo shule za sekondari za kutosha na kuwa na michepuo ikijumuisha elimu ya ufundi, kilimo na biashara kwa kuzipatia vifaa vya maabara.

Yahaya alitaja miradi iliyotekelezwa kuwa ni mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, matundu 10 ya vyoo uliogharimu Sh milioni 55 unaotekelezwa katika Shule ya Msingi Buhongwa.

Miradi mingine kwa shule za msingi ni ukamilishaji wa ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa Sh milioni 40 katika shule ya Buhongwa A.

Pia imejenga madarasa manne katika shule ya Mabatini B uliotumia Sh milioni 70 na ujenzi upo katika hatua ya kuezeka.

Mwingine ni ukamilishaji wa madarasa sita kwenye ujenzi unaoendelea katika shule ya msingi Mabatini A kwa Sh milioni 30 na ukamilishaji wa vyumba vitano vya madarasa katika shule mpya ya Swila na madarasa manne katika shule ya Majengo.

“Ujenzi huo unaendelea umefikia asilimia 50 kwa gharama ya shilingi milioni 35”, alisema na kuongeza kuwa ukarabati wa vyumba vya madarasa 13 na ofisi moja umefanyika katika Shule ya Msingi Nyanza English Medium kwa gharama ya Sh milioni 53.

Yahaya alitaja mradi mwingine ni wa utengenezaji wa madawati 200 katika shule ya msingi Ibanda  sanjari na ukarabati wa shule za msingi Nyegezi na Bulogoya kwa gharama ya Sh milioni 16.

Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa matundu ya vyoo 160 katika shule za msingi Bulale, Sahara, Ibanda, Igoma C , Nyakabungo, Mabatini B, Igogo A, Luchelele, Sweya na Kakebe ambapo ujenzi huo umekamilika.

Kwa elimu ya sekondari, alisema katika kipindi hicho, halmashauri ya jiji la Mwanza imetekeleza miradi ya thamani ya Sh 5, 292,167,022  kwa fedha kutoka serikali kuu, wahisani, mapato ya halmashauri, mapato ya halmashauri na michango ya wananchi.

Yahaya alisema jumla ya vyumba vya madarasa 103 (ghorofa 64 na vyumba vya kawaida 39) vimejengwa kwa upande wa sekondari kwa fedha za Covid-19 na mapato ya jiji. Sh bilioni 1.96 zilitolewa na serikali kuu na Sh 2.15 zimetokana na mapato ya ndani.

“Utengenezaji wa madawati 1,950 kwa shule za sekondari 13 umefanyika kwa gharama ya shilingi milioni 156”, alisema na kuongeza kuwa ukarabati wa madarasa matatu, maabara na vyoo matundu manane ulifanyika katika Shule ya Msingi Nyakurunduma kwa Sh 95,455,064.

Yahaya aliutaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa madarasa manane, ofisi mbili, jengo la utawala, makataba, jengo la Tehama, maabara tatu na vyoo matundu 20  katika shule mpya ya sekondari katika Kata ya Mkolani kwa Sh milioni 470 na ujenzi umefikia asilimia 90 ya utekelezaji.

Alisema miradi mingine ni ujenzi wa bweni , vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo kwa Sh 260,799,454 na ujenzi uko katika hatua ya boma. Shule sekondari Nganza imekarabatiwa kwa gharama ya Sh milioni 90 na ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nyakabungo vimekarabatiwa kwa Sh milioni nane.

“Tunaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa na ofisi za walimu katika shule za sekondari Bulale, Sahwa na Lwanhima ambao hadi sasa umetumia shilingi milioni 75 na ujenzi umefikia asilimia 90,” alisema.

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x