Miundombinu ya elimu Dar yazidi kuimarika

DAR ES SALAAM: Zaidi ya Sh bilioni 32 zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza miradi mbalimbali na ukarabati wa miundombinu ya elimu ya sekondari Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameyabainisha hayo leo Aprili 19, 2025 mara baada ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitunda ambao umegharimu Sh bilioni 4 .6.

Mpogolo amesema fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo yamekuwa chagizo ya ujenzi wa mradi huo wa ghorofa la kisasa.
“Sasa hivi halmashauri yetu inakwenda kuonuesha nguvu ya ukusanyaji wa fedha kwa ujenzi wa shule za kisasa kwani shule hii itakua ya ghorofa nne, madarasa 16, maktaba ya kisasa, maabara nne, ofisi 12 hivyo nampongeza Mkurugenzi wa Jiji kwa kuona umuhimu wa ujenzi wa shule za kisasa za ghorofa”,amesema Mpogolo.

Wakati huo huo amemtaka Mkurugenzi wa Jiji kuhakikisha mkandarasi wa mradi huo anakamilisha kwa wakati ifikapo Februari 2026, ili iweze kupokea watoto waliopo kwenye Kata ya Kitunda, Kivule Ukonga, Kipawa, na Kipunguni.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa Kwa Wananchi na utawezesha kutatua changamoto ya mrundikano wa wanafunzi madarasani ambao kwa sasa upo katika hatua ya ujenzi wa ghorofa moja.




